Friday, January 15, 2010

Udasa na sakata la Baregu

Chama cha Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (Udasa), leo kitatoa tamko kuhusu ajira ya Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Profesa Mwesiga Baregu, baada ya serikali kutamka rasmi kuwa haitamwajiri tena.

Waziri wa Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia, juzi alihitimisha mjadala huo kwa kueleza kuwa Profesa Baregu hawezi kuajiriwa kwa kuwa amekiuka Waraka Mkuu wa Utumishi No. 1 wa mwaka 2,000.

Alisema waraka huo unamkataza mtumishi wa umma kujihusisha na siasa na Profesa Baregu amekuwa kiongozi wa chama kwani ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa (Udasa), Josephat Rugemarila, alisema wanataaluma wanakutana leo chuoni hapo na baada ya mkutano huo watatoa tamko.

Akitoa mawazo yake binafsi, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekia Oluoch, alisema Waziri Ghasia amemwonea Profesa Baregu kwa kuwa kuna watumishi wengi wa umma ambao wanashikilia nafasi mbalimbali za siasa.

Alisema jana kuwa kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003 zinamruhusu mtumishi kujihusisha na siasa isipokuwa yamewekwa masharti ambayo mtumishi huo anapaswa kuyazingatia anapojiingiza katika siasa.

Oluoch aliyataja baadhi ya masharti hayo kuwa ni mtumishi huyo asitoe huduma kwa upendeleo, asitoe siri za serikali kwa chama chake, asihubiri sera za chama chake sehemu ya kazi na asifanye mambo ya siasa muda wakazi.

Aliongeza kuwa anachofahamu yeye ni kwamba Sheria ya Utumishi inawakataza kabisa askari polisi na wanajeshi kushiriki shughuli za kisiasa.

"Kwa maoni yangu, Waziri kamwonea Profesa Baregu maana kuna walimu lukuki ambao wako kwenye nafasi mbalimbali za kisiasa, katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Wako watumishi wa umma wameshinda nafasi za uongozi wa mitaa na vijiji na bado wako kazini, sasa kama ni Sheria au waraka iweje uwe kwa Profesa Baregu tu ," alisema.

Aliongeza kuwa watumishi hao hawaguswi kwasababu wameshinda nafasi hizo kupitia chama tawala (CCM), lakini wanaoshinda kupitia vyama vya upinzani ndio wanapata misukosuko.

"Kwa maoni yangu Waziri Ghasia aligadhabika, alikosa ushauri wa kisheria maana haiingii akilini sheria au kanuni imguse mtu mmoja tu," alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Said Arfi, alisema uamuzi uliochukuliwa na Ghasia dhidi ya Profesa Baregu, umeifadhaisha kambi ya upinzani nchini.

No comments:

Post a Comment