Tuesday, April 13, 2010

96 wahamishwa hospitali ya Mwananyamala.

Watumishi wapatao 96 wamehamishwa katika hospitali ya Mwananyamala na kuletwa watumishi wapya hospitalini hapo na waliokuwepo hapo wamesambazwa katika hospitali mbalimbali nchini.

Hatua hiyo imechukuliwa na Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam ambapo imeanza kusafisha Hospitali hiyo kwa lengo kufanya ufumbuzi hospitalini hapo.Jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw.William Lukuvi aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamefanya hivyo lengo ni kuboresha huduma zitolewazo hospitalini hapo.

Alisema uhamisho huo umegawanyika ambapo watumishi 57 wamehamishiwa katika hospitali za Dar es Salaam huku wengine 39 wamehamishiwa katika hospitali za mikoani.

Mbali na hilo tayari watumishi wapatao 58 kutoka hospitali zingine nchini wamepelekwa hospitalini hapo ili kubadilisha mtazamo na utendaji.

Alisema mbali uhamisho huo pia Serikali inabuni mbinu nyingine za kuiboresha kwa kuiongeza bajeti katika kipindi cha mwaka ujao wa fedha, ili kuboresha miundombinu na vitendea kazi na kusema uhamisho si njia pekee ya kuboresha huduma za Mwananyamala.

No comments:

Post a Comment