Sunday, April 11, 2010

Wanafunzi UDSM kutoa elimu-soko huria Afrika Mashariki.

Muungano wa wanafunzi wanaosoma taaluma ya fedha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUFA), chini ya Idara ya Fedha ya chuo hicho katika Shule ya Biashara, umepanga kutumia safari ya mafunzo nchini Kenya kutoa elimu ya kuwaondoa hofu Watanzania, kuhusu kujiunga na Shirikisho la Afrika Mashariki.

Hali kadhalika katika kujiunga na soko huria linalotarajiwa kuanza Julai mwaka huu.
Mwenyekiti wa muungano huo, Kenneth Ndulute, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa hatua hiyo inafuatia hofu iliyoonyeshwa na wananchi wengi, kuhusu uamuzi wa serikali wa kuingia katika soko huria.


"Tumepanga kutumia ziara yetu ya mafunzo nchini Kenya kuwatoa hofu na kuwapa moyo Watanzania kuhusu masuala ya Afrika Mashariki kwa jumla," alisema.

Kwa mujibu wa Ndulete, wananchi wengi hapa nchini, wanahofia kuporwa ardhi, dhana ambayo alisema haina msingi.
Alisema pamoja na soko huria lakini ardhi bado itaendelea kulindwa na sheria ya kila nchi na kwamba kwa msingi huo hakuna sababu ya Watanzania, kuingiwa na wasi wasi wa kuporwa ardhi yao.

Ndulute alisema katika safari hiyo, kundi la watu 50 litakalowakilisha muungano huo, litatembelea Chuo Kikuu cha Nairobi na kujifunza mchango wa sekta ya fedha kwa maendeleo ya sekta ya fedha ya Afrika Mashariki.

Alisema watu hao pia watajifunza kuhusu ujuzi wa soko la hisa na mitaji katika Soko la Hisa la Nairobi na kutembelea Benki ya Biashara ya Kenya (KCB) ambayo ni benki kubwa ya biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Ndulute alisema ziara hiyo pia itaboresha uhusiano kati ya wanafunzi wanaosoma masomo ya fedha katika vyuo hivyo.

No comments:

Post a Comment