Mhadhiri maarufu wa masuala ya kisiasa na kijamii, Prof Issa Shivji ameliponda baraza jipya la mawaziri akisema kuwa limeundwa kwa utashi wa kisiasa ili kulipana fadhila.
Prof Shivji, ambaye ni mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pia aliungana na wadau wengine wanaolilia mabadiliko ya katiba akisema suluhisho la matatizo mengi nchini ni kuundwa na katiba mpya itakayotokana na utashi wa wananchi.
Maoni yake yametokana na uteuzi wa baraza lenye mawaziri 50 uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete ambaye aliongeza mawaziri wapya 24 na kutema tisa baada ya kuchaguliwa kuongoza nchi kwa miaka mitano ya mwisho ya serikali ya awamu ya nne.
Baraza hilo lilianza kazi zake rasmi jana, lakini katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Channel Ten Shivji, ambaye amebobea kwenye sheria lakini ambaye amejishughulisha sana na siasa, alilizungumzia baraza hilo kuwa ni limeundwa kwa lengo la kulipa fadhila na si kwa kuzingatia uwezo.
“Kimsingi na kimantiki uteuzi na ukubwa wa baraza la mawaziri kwa nchi nyingi za Kiafrika na hata hili la Tanzania unatokana na utashi wa kisiasa hasa undugu na urafiki kwa lengo la kulipa fadhila," alisema Profesa Shivji.
"Mara chache uteuzi huzingatia mahitaji ya wananchi na maslahi ya taifa kwa ujumla. Ukubwa wa baraza si kipimo cha utendaji bora.’’
Profesa Shivji, ambaye alikuwa mhadhiri wa UDSM, alifafanua kwamba ndio maana wagombea ubunge walilazimika kumpigia debe mgombea urais wakati wa kampeni kwa lengo la kutaka kulipwa fadhila ya kuteuliwa kuwa waziri au naibu waziri
Alisema suala hilo pia linachochewa na sheria inayokazi9misha waziri ateuliwe kutoka miongoni mwa wabunge.
Profesa huyo alisema kimsingi kazi ya mawaziri ni kusimamia sera pamoja na utendaji na si vinginevyo.
Kikwete, ambaye aliunda baraza la mawaziri 60 alipoingia Ikulu kwa mara ya kwanza mwaka 2006, aliteua mawaziri watatu zaidi ya wale waliokuwemo kwenye baraza lililomaliza muda wake ambalo aliliteua mwaka 2008 baada ya Edward Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu.
Baraza hilo pia linaponekana kuzingatia uwakilishi wa kanda na mikoa na linajumuisha mabadiliko kadhaa ambayo mkuu huyo wa nchi aliyaelezea kuwa yamefanywa ili kuongeza ufanisi, ikiwa ni pamoja na kuhamisha baadhi ya idara kutoka wizara moja hadi nyingine na kuigawa Wizara ya Miundombinu kuwa katika wizara mbili.
Prof Shivji alisema kufanya mabadiliko ya muundo wa Baraza la Mawaziri bila kubadilisha mfumo ni sawa na kufanya bure.
Lakini alimshauri Rais Kikwete kuwa makini katika uteuzi wa makatibu wakuu wa wizara pamoja na manaibu wao, akimtaka azingatie uwezo katika utendaji.
“Katibu mkuu ndiye mtendaji wa shughuli za kila siku za wizara. Kazi ya waziri ni kusimamia sera na utendaji tu," alisema Prof Shivji.
“Rais Kikwete anatakiwa kufanya kazi ya ziada katika kuteua makatibu wakuu... muhimu ni lazima wawe wasomi wazuri, wenye uwezo na watakaokuwa wepesi wa kuelewa wanachoshauriwa na wataalamu,’’ alisema Profesa Shivji
Profesa huyo alisema kulingana na hali ya uchumi ilivyo nchini, serikali ya Kikwete inakabiliwa na changamoto nyingi hasa ya kuhakikisha nchi inazalisha zaidi kuliko ilivyo sasa.
Alisema pamoja na kwamba asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima, sekta hiyo inachangia katika pato la taifa kwa asilimia 26, akifafanua kuwa kiwango hicho kinamaanisha kuwa Watanzania wanazalisha kwa asilimia 26.
Mhadhiri huyo ambaye ni mwanaharakati wa ardhi alisema katika miaka ya 50, kilimo nchini kilifanya vizuri na nchi ilikuwa ikizalisha kwa wastani wa zaidi ya asilimia 50, lakini kiwango hicho kimekuwa kikishuka kila mwaka.
“Ukiniuliza sababu ya hili, nitakueleza tu kuwa tumeua kwa makusudi viwanda vyetu pamoja na kilimo,’’ alisema
Alifafanua kwamba ili nchi yoyote iweze kuendelea, ni lazima uzalishaji wake uwe mkubwa na hasa kutoka kwa wazalishaji wadogo wa vijijini na kwamba uchumi unayumba kutokana na wazalishaji wadogo kutothaminiwa.
Alisema ili nchi ipige hatua ya kimaendeleo ni lazima kilimo cha umwagiliaji kipewe nafasi kubwa pamoja na kuwepo kwa zana za kisasa za kilimo, ikiwa ni pamoja na wakulima kukopeshwa fedha kutoka katika benki.
“Wanasema Tanzania ni maskini lakini cha ajabu ina benki nyingi tena za kimataifa ambazo haziko tayari kuwakopesha wakulima,’’ alisema.
“Serikali ndio ilipaswa kuwa dhamana kwa wakulima kukopa lakini haiko tayari katika hilo.’’
Gwiji huyo wa sheria na aliyebobea katika masuala ya katiba alikwenda mbali na kusema pamoja na mambo mengine suluhisho la matatizo mengi nchini ni kuundwa kwa katiba mpya itakayotokana na utashi wa wananchi.
Profesa Shivji alisema kinachopaswa kuzingatiwa kwa sasa ni ni jinsi katiba hiyo itakavyoundwa ili iweze kupata uhalali wa wananchi wote.
“Hapa napenda wananchi waelewe kuwa unapozungumzia katiba mpya, huzungumzii muundo wake bali jinsi inavyotungwa ili iweze kupata uhalali wa wananachi wote na si tu yale yatakayokuwemo ndani yake,’’ alisema
Alifafanua kwamba katiba ya sasa ambayo ni ya mwaka 1977, ilitokana na mfumo wa kisiasa wa chama kimoja pamoja na hivyo kushirikisha watu wachache.
Alisema hali hiyo inaifanya katiba iwe haikidhi utashi wa Watanzania walio wengi kutokana na kwamba haiendani na mazingira ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni yalivyo sasa.
Alitoa mfano wa katiba mpya ya nchini Kenya ambako alisema ilitokana na wananchi na kwamba pamoja na mambo mengine imepunguza madaraka ya rais, ikiwa ni pamoja na ukubwa wa Baraza la Mawaziri kutokana na kueleza bayana kuwa lisiwe na chini ya watu 14 na lisizidi watu 24.
“Wamekwenda mbali zaidi na sheria kutaka wanaoteuliwa kuwa mawaziri wasiwe wabunge, bali wathibitishwe na Bunge,’’ alisema .
Lakini Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani alikaririwa jana akisema kuwa serikali haijawa tayari kuunda katiba mpya na kwamba itaendelea na mtindo wa kufanya marekebisho ya sheria hiyo wakati wowote itapolazimika.
Wednesday, December 1, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment