Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee, jana alifichua ufisadi katika sekta ya ardhi, huku akiituhumu kampuni ya kigeni iliyotumia leseni ya uwindaji,kuchimba madini.
Akiwasilisha maoni ya kambi yake kuhusu hotuba ya makadirio ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mdee alisema kuna kila dalili kwamba Tanzania imegeuzwa kuwa shamba la bibi kwa sababu kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria za nchi.
Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema), alisema mkataba baina ya kampuni ya Uranium Resourses PLC, Western Metals Limited na Game Frontiers of Tanzania Limited, ni ushahidi wa kuwapo kwa madudu mengi yanayofanyika huku Serikali ikiyafumbia macho.
Alisema mkataba huo wa siri, umetengenezwa na Kampuni ya Uwakili ya Rex Attorneys ulisainiwa Machi 3 mwaka 2007 na kwamba unaruhusu kampuni za uwiandaji kufanya uchimbaji wa madini ya Uranium katika Kijiji cha Mbarang’andu.
Mdee alisema Kampuni ya uwindaji ya Game Frontiers of Tanzania Limited inayomilikiwa Mohsin M. Abdallah na Nargis M. Abdallah, imeingia mkataba na kampuni mbili za kigeni zinazofanya utafiti wa uchimbaji wa madini ya Uranium katika kijiji hicho.
Mdee alisema mkataba huo ni wa malipo ya Dola 6 milioni za Marekani milioni 6 ambazo zitalipwa kwa awamu mbili ya malipo ya Dola 3 milioni kwa kila awamu.
“Malipo ya kwanza yatafanyika pale uzalishaji wa Uranium utakapoanza.
Malipo ya Dola 250,000, yatafanyika baada ya kampuni za madini kukamilisha utafiti wa madini ya urani na kupata kibali cha uchimbaji wa madini,”alisema Mdee.
Aliyataja malipo mengine kuwa ni Dola 55,000 za Marekani kila mwaka kama fidia ya kushindwa kufanya biashara na usumbufu unaotokana na shughuli za machimbo kwenye kitalu na kwamba malipo hayo yatafanyika kila Mach 31.
Mengine ni Dola 10,000 za Marekani kwa vijiji vitakavyoathiriwa na utafiti huo wa urani, malipo ambayo yametokana na makubaliano baina ya kampuni ya uwindaji na kampuni za madini.
“Nimepitia sheria za uhifadhi wa wanyamapori, The wildlife Conservation Act, 1974 (Sheria ya zamani) na Sheria mpya The wildlife Conservation Act, Act no 5 of 2009. Sheria hizi zinamruhusu mtu aliye na leseni ya uwindaji, kuwinda wanyama tu,”alisema Mdee na kuongeza:
“Hali kadhalika, Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999, Sheria namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi ya vijiji, sheria namba 5 ya mwaka 1999 inatamka bayana kwamba ardhi inajumuisha vitu vyote vilivyo juu ya ardhi na chini ya ardhi isipokuwa madini au mafuta na gesi”.
Alihoji sababu za kukiukwa kwa taratibu za nchi zinazoelekeza kwamba linapokuja suala la madini, umiliki unatoka kwa mtu binafsi na kurudi serikalini nakwamba Wizara ya Nishati na Madini ndiyo pekee yenye mamlaka ya kutoa leseni ya kutafuta madini kwa kampuni za madini!
“Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ilieleze Bunge lako tukufu uhalali wa mkataba kati ya Game Frontiers na Uranium Resourses PLC na Western Metals! Ni sheria ipi inayoipa kampuni ya uwindaji haki ya kualika kampuni ya nje kwenye eneo ambalo haina umiliki kufanya utafiti na hatimaye kuchimba madini hatari kama urani,,”alihoji.
Thursday, July 12, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment