Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Felloship (FGBF), Zachary Kakobe amesema ufisadi nchini hauwezi kumalizika iwapo nchi itaendelea kuongozwa na mafisadi.
Akihubiri katika Ibada kwenye kanisa hilo lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam juzi Jumapili, Kakobe aliwataka waumini wake kujiunga katika vyama vya siasa na kugombea nafasi za uongozi ili waiongoze nchi.
Alisema kwa sasa nchi inatawaliwa na mafisadi na ndio sababu wamejenga dhana ya “chukua chako mapema” kwa kukosa hofu ndani ya mioyo yao kwa uovu wanaowatendea wanyonge.
“Wote wanaoimba wimbo wa ufisadi ni wanafiki wakubwa, tena ndio mafisadi wenyewe. Mwenyehaki akitawala baraka za Mungu zinakuja na nchi inastawi”, alisema Kakobe.
Kakobe alisema wenyehaki wakijitosa katika siasa kwa nguvu zote wataushinda ufisadi, lakini, wakikaa pembeni, ufisadi hautakwisha na kwamba nchi itaendelea kutawaliwa katika misingi ya kifisadi.
“Mwenye haki ndiye anapaswa kuongoza, kwa sababu atasimamia haki za wanyonge, tofauti na sasa nchi inavyoongozwa ambapo kuna watu zaidi ya milioni nane hawajui watakula nini, kwa sababu nchi haiongozwi katika misingi ya sheria ya Mungu”, alisema.
Askofu huyo alisema viongozi wanaoongoza nchi hawana hekima kwa sababu hawaongozwi na Neno la Mungu, tofauti na alivyokuwa hayati Julius Nyerere aliyesema alikuwa akitembea na Biblia kila alipokwenda iliyompatia hekima katika utawala wake.
“Aliye mkamilifu anayo hekima ndani yake, nahitaji watu wenye haki wajiunge na siasa ili ufisadi uondoke kabisa katika nchi hii na wanyonge wapate haki zao”, alisema Kakobe.
Kakobe aliwataka waumini wake kujinga katika vyama mbalimbali vya siasa akieleza kuwa, hata Yesu alikuwa upande wa wapinzani na kwamba msemo wa ‘fikra kwa mwenyekiti zidumu’ sasa haupo tena.
“Jiunge na chama tawala, hata CCJ ingia nitakutia mafuta. Watu wanaosema siasa ni mchezo mchafu, wachafu ni wao wenyewe, tangu sasa dhamiria kuingia kwenye siasa”, kiongozi huyo alisema.
Kakobe alisema yeyote mwenye haki atapata ujasiri kama simba katika kupambana na mafisadi na kwamba hata yeye anao ujasiri aliosema amepata kutoka kwa Mungu.
Kakobe aliyewahi kulumbana na serikali katika mambo kadhaa, alisema viongozi wanaoongoza bila kuwa na hofu mioyoni mwao wanatawaliwa na nguvu za giza.
Alisema kwamba miungu ya viongozi ni tofauti na wenye haki wanaoongoza kwa sheria na misingi ya Mungu.
"Wanaoongoza bila hofu ya Mungu, muingu yao iko Bagamoyo, Sumbawanga na Pemba, tofauti na wenye haki ambao wataongoza na sheria inayotengenezwa na misingi ya Mungu",alisema.
Alisema shetani daima anataka watu wanaofanya matambiko na kwenda kwa waganga waongoze nchi, ili waendelee kufanya maisha ya wanyonge yaendelee kuwa magumu na wasijue watakula nini", alisema Kakobe.
Hata hivyo, alisema kuwa wapo watawala wanaotafsiri vibaya Neno la Mungu wakidhania kwamba mtu mcha Mungu hatakiwi kutawala, bali kutawaliwa na kueleza kuwa dhana hiyo ni uongo na potofu akisema, biblia haitafsiriwi jinsi mtu aonavyo.
Tuesday, June 1, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment