Thursday, July 8, 2010

Waliokuwa wafanyakazi Tazara wakata rufani.

Wafanyakazi 152 wa zamani wa Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (Tazara) waliostaafishwa na mwajiri wao mwaka 2001, wamekata rufani Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakipinga uamuzi huo.

Rufani ya wafanyakazi hao inatokana na kutokuridhika na uamuzi wa Mahakama ya Kazi pamoja na marejeo ya jopo la mahakama hiyo lililoridhia kuwa wafanyakazi hao walistaafishwa kihalali.


Pia Jopo hilo lililoongozwa na Mwenyekiti wa mahakama hiyo Jaji Ernest Mwipopo katika uamuzi wake uliotolewa April 27 mwaka jana lilisema kuwa waomba marejeo hao hawana madai zaidi kwa mwajiri wao kwa kuwa tayari walishalipwa mafao yao.

Katika rufani yao, kiongozi wa wafanyakazi hao, Sylvester Dagaa kwa niaba ya wenzeke 151 waliiomba mahakama itengue maamuzi ya mahakama ya kazi na iamuru kuwa walistaafishwa kinyume cha sheria na wana haki ya kulipwa stahili zao.


“Jopo la marejeo la Mahakama ya Kazi lilikosea kiukweli na kisheria kusema kuwa warufani waliondolewa katika ajira kisheria baada ya kufikisha umri wa kustaafu kwa lazima wa miaka 55, ” walidai katika hati yao ya rufani na kuongeza;

“Jopo la marejeo la mahakama hiyo ilikosea kisheria na kiukweli kusema kuwa warufani walikuwa wameshalipwa mafao yao yote kwa mujibu wa rufani na hivyo hawana madai mengine zaidi na kwamba hakuna hasara yoyote waliyoipata”.

Pia warufani hao wanadai kuwa jopo la marejeo la mahakama hiyo lilikosea kisheria na kiukweli kusema kuwa kwa kuwa warufani waliondolewa katika ajira kisheria, na kulipwa mishahara yao ya miezi 24 kama fidia, walilipwa isivyo halali.


Katika hati yao, warufani hao pia wanapinga uamuzi wa jopo hilo la marejeo kwamba mahakama hiyo haina uwezo wa kuamuru kulipwa kwa fidia kutokana na upande wowote kuvunja mkataba moja kwa moja ama kwa dokezo.

Kutokana na sababu hizo warufani hao sasa wanaiomba Mahakama Kuu itengue uamuzi wa jopo la Mahakama ya Kazi na itamke kuwa mjibu rufani alivunja masharti ya mkataba wa ajira na waomba rufani na kwamba walistaafishwa kinyume cha sheria.

Pia wanaiomba Mahakama Kuu itamke kuwa wajibu rufaa hao, wamepata madhara maalumu na ya jumla,kutokana na mjibu rufaa kuvunja mkataba wa ajira. Sambamba na hayo wanaiomba mahakama hiyo itamke kuwa wanastahili kulipwa fidia zaidi ya iliyoamriwa na Mahakama ya Kazi katika uamuzi wa awali, kadri mahakama hiyo itrakavyotathmini, pamoja na gharama za rufaa. Katika shauri la msingi namba 42 la mwaka 2005, Mahakama ya Kazi katika uamuzi wake wa Septemba 28 ilitupilia mbali madai ya walalamikaji hao.

Mahakama hiyo ilisema kuwa kustaafishwa kwa lazima kwa umri wa miaka 55 ni sahihi kwa kuzingatia mkataba wa hiyari kati ya walalamikaji, mwajiri na Chama cha Wafanyakazi (Trawu), na badala yake iliagiza walipwe mishahara yao ya miezi 24 tu.


Hata hivyo walalamikaji hao hawakuridhika na uamuzi huo kwa madai kuwa mkataba huo wa hiyari baina ya walalamikaji na mwajiri unakinzana na sheria za nchi hususan Sheria ya Kazi, ndipo walipoomba uamuzi huo ufanyiwe marejeo.

Jopo la marejeo la mahakama hiyo lilikubaliana na uamuzi wa mwanzo, lakini likaenda mbali zaidi na kusema kuwa kwa kuwa walistaafishwa kisheria hawakustahili malipo ya miezi 24 waliyokuwa wamelipwa, uamuzi ambao umesababisha wakate rufani Mahakama Kuu.

No comments:

Post a Comment