Thursday, August 5, 2010

Rushwa CCM inatisha-UNDP

Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), limesema rushwa iliyojitokeza katika mchakato wa kura za maoni za CCM, ni hatari kwa mustakabali wa taifa.

Kufuatia hali hiyo shirika hilo limewataka Watanzania hasa vijana, kutokubali kununuliwa katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
“Katika vitu vya kushangaza ni jinsi wagombea ubunge na udiwani wa CCM walivyokuwa wakishindana kutoa rushwa ili wachaguliwe na wananchi,” alisema Meneja Mradi wa Kusaidia Uchaguzi wa UNDP, Oskar Lehner.


Lehner alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika kongamano la siku mbili lililowakutanisha zaidi ya vijana 140 kutoka mashirika mbalimbali yasiyokuwa ya kiserikali na wale wa vyuo vikuu.

Kwa mujibu wa Lehner, uuzaji wa shahada za kupigia kura katika uchaguzi, ni sawa na kuuza malengo ya baadaye katika maisha ya watu hivyo ni vyema Watanzania wakafahamu kwamba mustakabali wa maendeleo ya nchi upo katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu.

UNDP inatoa kauli hiyo baada ya vyombo mbalimbali vya habari kuripoti rushwa katika mchakato mzima wa kura za maoni za CCM kuwapata wabunge na madiwani watakaogombea katika uchaguzi ujao.


“Angalieni jinsi matendo ya rushwa yalivyoripotiwa katika mchakato wa kampeni na upigaji kura za maoni ya kuchagua mgombea ubunge na udiwani wa CCM," alisema na kuongeza.

“Wananachi na hasa vijana mjihadhari na kujiepusha na rushwa katika uchaguzi, eleweni kuwa, kuuza shahada yako ya kupigia kura, ni sawa na kuuza malengo ya baadaye katika maisha yako,"
“Mafanikio na maendeleo ya baadaye ya nchi, yapo katika mikono yenu hasa katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu.”


Akizungumzia malengo ya kongamano hilo, Lehner alisema mpango mkakati ni kuwajengea uwezo vijana ili waweze kutoa sauti na kujua umuhimu wa kupiga kura katika chaguzi na kudhibiti rushwa.

“Tunahitaji vijana wawe na sauti, kuleta mtazamo mpya katika jamii na nchi kwa ujumla. Uchaguzi uwe wa haki na uwazi kwa umma na vijana watambue umuhimu wao katika jamii,’’ alisema Lehner.

Lehner alisema, katika kuhakikisha wanadhibiti rushwa katika chaguzi, wameanzisha mpango maalumu wa kukuza ubora wa vyombo vya habari ambapo watatoa mafunzo maalumu kwa wanahabari.

Awali mratibu wa kongamano hilo, Humphrey Polepole alisema pamoja na mambo mengine, kongamano hilo pia limelenga kuwafunda vijana, wasihadaike na hongo zinazotolewa na wagombea.

Pia wanataka vijana waweze kuhimili mashinikizo ya kuwachagua wagombea kwa matakwa ya watu wengine.

Polepole ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tanzania Youth Coalition (TYC) alisema, katika kongamano hilo kuwa mbali na kupiga kura katika chaguzi, vijana pia wataandaliwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

“Kongamano kama hili tutalifanya Visiwani Zanzibar mwishoni mwa mwezi huu,” alisema Polepole.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Maendeleo ya Vijana Tanzania (Yuneda), Murshid Ngeze, alisisitiza elimu hiyo kutolewa zaidi kwa vijana wa mitaani na watu wa kada ya chini ambao kwa asilimia kubwa, ndio wanaorubuniwa na wagombea wakati wa chaguzi.

“Pamoja na kwamba tatizo la uelewa kwa vijana ni kubwa, elimu kama hii ingetolewa kwa watu wa kada ya chini kwani wao ndio wanaorubuniwa kiurahisi kutokana na kutokuwa na uelewa wa mambo ya chaguzi,’’ alisema Ngeze.

Mkurugenzi huyo alisema kulingana mazingira yalivyo nchini, vijana wengi wanafanya mambo pasipo kuchambua na kwamba hilo linatokana na kuwa na uelewa mdogo unaotokana na kutoandaliwa pamoja na kutojua fursa mbalimbali zilizoandaliwa na serikali.

Matokeo ya kura hizo, zimewaangusha wabunge waliokuwa wakitetea nafasi zao zaidi ya 65, wakiwamo mawaziri.

Kongamano hilo lilihusu utoaji wa elimu ya uraia na pamoja na umuhimu wa jamii na hasa vijana kupiga kura.

No comments:

Post a Comment