Udanganyifu katika mitihani ya taifa ya kidato cha nne inayoendelea nchini umeendelea baada ya mwalimu wa Shule ya secondari Mbezi, Presidia Rwebugisa, 44, na mwanafunzi Ritha Daniel, 18, kupandishwa kizimbani jijini Dar es salaam kujibu tuhuma za kula njama na kufanya udanganyifu.
Watuhumiwa hao, ambao wote ni wakazi wa Mbezi Luis jijini Dar es Salaam, walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Karim Mushi.
Mwendesha mashtaka wa polisi, Mrakibu Naima Mwanga alidai mahakamani hapo kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Oktoba 6 mwaka huu kwenye Shule ya Sekondari ya Tambaza jijini Dar es Salaam.
Mwanga alieleza kuwa katika shtaka la kwanza watuhumiwa wote kwa pamoja katika muda na wakati usiofahamika, walikula njama kutenda kosa hilo.
Mwanga alidai katika shtaka la pili kuwa mtuhumiwa wa pili, Ritha Daniel, ambaye ni mwanafunzi, alijifanya kuwa ni mmoja wa watahiniwa wakati akijua kuwa si kweli.
Alieleza kuwa siku ya tukio majira ya saa 9:00 alasiri, mtuhumiwa huyo aliingia katika kituo cha kufanyia mitihani kilichopo Shule ya Sekondari ya Tambaza kwa lengo la kumfanyia mtihani mtuhumiwa wa kwanza kinyume cha sheria.
Hata hivyo, hakufafanua kuwa mshtakiwa huyo wa pili ni mwanafunzi wa shule gani.
Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka huyo, mwanafunzi huyo aliingia kwenye chumba cha mtihani kwa nia ya kumfanyia mtihani mwanafunzi mwingine ambaye mtahiniwa binafsi katika kituo cha Tambaza na akatumia jina la Prasidia huku akijua kuwa si kweli.
Watuhumiwa wote walikana mashtaka na kuachiwa kwa dhamana hadi Oktoba 25 mwaka huu baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili; mmoja mwajiriwa wa serikali ambao wote wametakiwa kusaini dhamana ya ya Sh2 milioni kila mmoja.
Hili ni tukio la pili linalohusiana na mtihani wa kidato cha nne kufikishwa Mahakama ya Ilala.
Oktoba 8 mwaka huu, Mwalimu Majaliwa Lemnyambwa, 34, mwanafunzi Habiba Kambwili, 25, na mkazi wa Tandika Matrida John, 25, walikamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kufanya mitihani hiyo bila kusajiliwa.
Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Esther Mwakalinga.
Mwendesha mashtaka wa polisi, Mkaguzi Mussa Gumbo alidai mahakamani hapo kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti Oktoba 4, mwaka huu kwenye Shule ya Sekondari ya Tabata.
Alidai siku ya tukio saa 5:30 asubuhi, mwalimu huyo wa twisheni, aliingia chumba cha mtihani akitumia jina la Seleman Kimaro kuonyesha kuwa yeye ni mwanafunzi wa kidato cha nne mwenye namba P. 1310/0254.
Gumbo aliendelea kudai kuwa Kambili, ambaye ni mtuhumiwa namba mbili, alitenda kosa hilo siku hiyo hiyo saa 3:45 asubuhi.
Aliieleza mahakama kuwa siku hiyo mtuhumiwa huyo aliingia chumba cha mtihani akionyesha kuwa yeye ni Jackline Barukina mwenye namba ya mtihani P. 1310/0047.
Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka huyo, Matrida John, ambaye ni mshtakiwa wa tatu, anakabiliwa na kosa la aina hiyo baada ya kujifanya anaitwa Theresia Mfubusa mwenye namba ya mtihani P. 1310/0131.
Hata hivyo watuhumiwa hao wamekana kosa na kurudishwa rumande hadi Oktoba 22 baada ya kukosa dhamana
Tuesday, October 12, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment