Tamko la mnadhimu mkuu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo bado linakosolewa baada ya waangalizi wa uchaguzi mkuu kutoka Jumuiya ya Umoja wa UIaya (EU) kulaani kitendo hicho, wakieleza kuwa kimevuka mipaka ya shughuli za chombo hicho.
Akitoa tamko hilo Oktoba mosi, Shimbo aliwaambia waandishi wa habari kuwa vyama vya siasa havina budi kukubali matokeo ya uchaguzi mkuu yatakayotangazwa baada ya upigaji kura na kwamba vyombo vya usalama vimejiandaa kikamilifu kupambana na yeyote atakayejaribu kuyakataa.
Hata hivyo, serikali imekuwa ikimtetea Shimbo kwa kusema kuwa alitoa tamko hilo kama kiongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ma si kama kiongozi wa jeshi na kwamba kitendo alichofanya ni sahihi.
Badala yake, tamko hilo lilipingwa na vyama vya siasa, taasisi za kijamii na wasomi ambao walitafsiri kuwa ni vitisho dhidi ya wapigakura na kwamba lililenga kulinda ushindi usio wa haki.
Jana, mwangalizi mkuu kutoka tume ya Ulaya inayoshuhudia uchaguzi mkuu nchini, David Martin alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa kazi ya kuonya dhidi ya vurugu wakati wa kampeni inatakiwa ifanywe na Tume ya Uchaguzi (Nec).
“Kauli hiyo ilitolewa kimakosa kwa kuwa zipo tume za uchaguzi... inakuwaje tena JWTZ kuhusika kutoa kauli kali kama hizi tena katika kipindi hiki cha uchaguzi,” alihoji Martin.
Martin alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kazi yao ya kuangalia mwenendo wa uchaguzi mkuu ambao umepangwa kufanyika Oktoba 31 na ndipo alipoulizwa swali kuhusu tamko hilo la Shimbo.
Martin alisema kuwa ujumbe wake umekuja kutathmini kwa kina mchakato mzima wa uchaguzi na kuangalia kiasi gani uchaguzi unaheshimu kanuni za kimatiafa zinazotawala chaguzi za kidemokrasia na sheria za nchi.
Kwa mujibu wa Martin ujumbe huo unaohusisha Kamisheni ya Ulaya, Baraza na Bunge la Ulaya ni tume huru inayofanya kazi zake bila kukipendelea chama chochote cha siasa.
“Tuko hapa kwa ajili ya kuendesha shughuli zetu kwa uhuru bila kuegemea au kupendelea upande wowote,” alisema.
Martin alieleza kuwa jukumu la msingi lililowaleta nchini ni kuangalia mchakato mzima wa uchaguzi na kwamba baadaye watatoa ripoti maalumu ya kitaalamu ambayo alisema itakayosaidia ukuaji wa demokrasia nchini.
Alieleza kuwa siku ya uchaguzi kutakuwa na kikundi cha wataalamu sita wakishirikiana na waangalizi 22 wa muda mrefu, na wengine 42 wa muda mfupi ambao kwa pamoja watakuwa wakifuatilia zoezi la upigaji kura Bara na Visiwani.
"Kazi ya watalaamu hao ni kuangalia tu na hawatatenda chochote ambacho kitaweza kuingilia au kushawishi uchaguzi kwa kuwa si jukumu la tume hii," alisema Martin na kuongeza:
“Lakini nategemea kuwa ripoti yetu ya mwisho ambayo tutaiwasilisha kwa viongozi wa Tanzania miezi miwili au mitatu baada ya uchaguzi, itawasaidia kwenye maamuzi ya mustakabali wa demokrasia ya nchi yenu,” alisema.
Wakati akitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari Agosti mosi, Shimbo alikuwa ameambatana na naibu kamishna msaidizi wa Jeshi la Polisi, Peter Kivuyo na mkuu wa Operesheni Maalum (DCP), Venance Tossi.
Siku hiyo, Shimbo alisema: “Tuko tayari kupambana na yeyote yule; kuna matamshi makubwa yanatolewa kuwa damu itamwagika; hakuna damu itakayomwagika na wala hatutaruhusu jambo hilo kutokea na asitokee mtu akajaribu kufanya hivyo; uchaguzi umeanza vizuri na uishe vizuri.”
Kwa mujibu wa Luteni Jenerali Shimbo, vyama vya siasa, wagombea na wapambe wao wanapaswa kufanya kampeni kwa ustaarabu na kwa kufuata sheria na kanuni za uchaguzi zilizopo.
Pamoja na kueleza kuwa kuna wanasiasa ambao wanatoa matamko ya uchochezi, hadi sasa Jeshi la Polisi halijamkamata mtu yeyote na kumuhusisha na tuhuma za uchochezi, jambo ambalo kisheria ni kosa.
Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa amekuwa akipa changamoto Jeshi la Polisi kukamata wanasiasa ambao wanatoa kauli zinazoonekana zinalenga kumwaga damu badala ya kutoa vitisho.
Kauli ya Martin imekuja siku chache baada ya Mtandao wa Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu (FemAct) kutoa tamko la kulaani kitendo hicho.
Mbali na kulaani tamko hilo FemAct, ambayo imeundwa na mashirika 50 yasiyokuwa ya kiserikali, ilisema inaamini kauli hiyo ya Shimbo haikutolewa bure bali kwa msukumo wa chama fulani cha siasa.
Wednesday, October 13, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Kwa kipindi kama hiki nafikiri wanausalama wangejaribu kuangalia nini wanachokiongea, na kama ni lazima kukemea jambo fulani wangetumia njia ambayo haitaleta uonekanaji wao kuwa wanaegemea wapi,najua wanajua kuwa wao kwa sasa ndio mlinzi wa serikali na sio chama...
ReplyDeletewell said emu-three
ReplyDelete