Tuesday, April 28, 2009

vita dhidi ya mafisadi tz yazua malumbano miongoni mwa vigogo wa serikali!

MAWAZIRI wawili, Sophia Simba na George Mkuchika jana walimshambulia mfanyabiashara maarufu nchini, Reginald Mengi ambaye wiki iliyopita alitangaza majina ya wafanyabiashara watano wenye asili ya Kiasia, akisema ni mafisadi waliokubuhu.

Simba, ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) na Mkuchika, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo walisema mfanyabiashara huyo wa jijini Dar es salaam "amechemsha".

Mengi alitangaza majina ya wafanyabiashara hao Alhamisi iliyopita akisema ni kati ya watu wasiozidi 10 ambao alidai wanaifilisi nchi na kutaka wadhibitiwe mapema kabla hawajaitingisha na kuiyumbisha nchi.

Hata hivyo, Mengi, ambaye alidai katika taarifa yake kuwa juhudi za Rais Jakaya Kikwete zinakwamishwa na watu hao, hakueleza jinsi watano hao wanavyoitafuna nchi zaidi ya kusema kuwa wanatorosha fedha wanazozipata 'kifisadi'.

Jana, kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam mawaziri hao wawili walitoa kauli za kumshambulia mwenyekiti huyo mtendaji wa makampuni ya IPP, kauli ambazo zinadokeza mtazamo wa serikali katika mjadala unaoendelea wa vita dhidi ya ufisadi na vinara wake.

Waziri Simba, ambaye wizara yake pia inawajibika katika vita dhidi ya ufisadi, alisema: "Kakosea... watoto wa mjini wanasema kachemsha."

Simba alitoa msimamo huo jijini Dar es Salaam jana muda mfupi baada ya kufungua semina ya wadau wa vyama vya siasa kuhusu namna ya kuiboresha Sheria ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995.

Simba alisema Mengi hana mamlaka hayo ya kutaja watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Kabla ya kujibu swali kuhusu kitendo cha Mengi, ambaye anamiliki televisheni ya ITV na kituo cha redio cha Radio One Stereo, kutaja majina ya watu hao aliowaita mafisadi papa, Simba alihoji: " Hapa kuna mtu wa ITV?."

Baadaye alisema: "Sikilizeni, kwanza kitendo alichokifanya Mengi si sahihi, kakosea hawezi kuhukumu watu, mamlaka hayo anatoa wapi?"

Simba, huku akionekana kama mtu ambaye alikuwa akitafuta jukwaa kuzungumzia suala hilo, alisema Mengi amekosea kwa kuwa baadhi ya watu aliowataja wana kesi mahakamani.

"Anahukumu watu," alisema. "Kuna mtu kama Jeetu (Patel) ana kesi mahakamani (EPA), sasa unapokuja kusema ni fisadi wakati mahakama haijathibitisha, unakuwa na maana gani.

"Kwanza kwanini awatuhumu wafanyabiashara wenzake tu, ina maana si ana nia mbaya nao."Alisema Mengi amechukua uamuzi huo kama vile serikali, wakati serikali ipo siku zote na imekuwa ikifanya kazi zake kwa umakini kwa kufuata misingi ya sheria.

"Serikali ipo na inafanya kazi kwa misingi ya sheria, sasa yeye kukaa na kutangaza watu nasema si sahihi kabisa. Mahakama pekee ndiyo inaweza kumtia mtu hatiani, lakini huwezi kuhukumu watu kama hakuna mamlaka."

Waziri Simba, ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), alisema Mengi hapaswi kutumia vyombo vyake vibaya.

"Asitumie vyombo vyake kufanya atakavyo yeye. Huwezi kukaa katika chombo chako na kuanza kuhukumu watu. Kila mtu akifanya hivyo itakuaje," alihoji.

Akiongea na Mwananchi baada ya kupata taarifa za kauli ya Simba, Mengi alisema: "Namuombea kwa Mwenyezi Mungu na kwa maskini wa Tanzania ili wamsamehe kwa sababu hajui anenalo."Mengi hakutaka kuzungumza zaidi kuhusu hatua hiyo ya Mama Simba.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika aliwaambia waandishi wa habari kuwa serikali itamchukulia hatua za kisheria Mengi iwapo itabainika alikiuka taratibu na kanuni za nchi kwa kutangaza majina ya watu anaowatuhumu kwa ufisadi.

Mkuchika alisema jijini Dar es Salaam jana kwa sasa serikali inafanya uchunguzi juu ya suala hilo na itatumia mikanda ya video pamoja na maelezo ya kimaandishi aliyoyatoa Mengi siku alipokutana na waandishi wa habari.

"Tumekusudia kupata ule mkanda wa video, pia tusome maelezo yake ya kimaandishi... tukigundua kuna mahala ambapo sheria haikuzingatiwa, (Mengi) atachukuliwa hatua," alisema Mkuchika.

Mkuchika alisema serikali imepokea malalamiko mengi kutoka kwa watu wengi, wakishutumu hatua iliyochukuliwa na Mengi, ambaye pia anamiliki viwanda vya vinywaji.

Bila kutaka kuwataja majina, Mkuchika alisema miongoni mwa walalamikaji, wapo walioeleza kuwa vyombo vya habari vya mfanyabiashara huyo havikuwatendea haki watuhumiwa waliotajwa kuwa ni mafisadi wakuu.

Alisema ni kutokana na vyombo hivyo kuwataja majina watuhumiwa bila ya kuwapa fursa ya kujibu madai dhidi yao.

Waziri Mkuchika alipotakiwa kueleza siku ambayo uchunguzi huo utakamilika, alijibu wananchi wanapaswa kuwa watulivu kwa sababu serikali ikimaliza kuchunguza, itawatangazia yale waliyobaini.

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miezi takribani mitatu kwa Mengi kuingia katika mvutano na serikali baada ya kuvutana mapema mwaka huu na Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha kutokana na kutangaza kuwa kuna mipango ya kumfilisi na kumuua.

Mengi pia amewahi kujikuta katika malumbano na watendaji wa serikali hasa na waziri wa zamani wa nchi, ofisi ya rais (utawala bora), Wilson Masilingi alipotoa tuhuma kuwa suala la utoaji zabuni ya ununuzi wa hoteli ya Kilimanjaro, hivi sasa inajulikana kama Kilimanjaro Kempiski, kulikuwa na kitu alichokiita "mchezo mchafu".

Suala hilo liliamsha malumbano makali, lakini liliishia hewani.

Katika tuhuma za wiki iliyopita, Mengi aliwahusisha wafanyabiashara hao watano na kashfa za wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), utoaji zabuni ya ufuaji umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond Development (LLC) na uuzwaji wa jengo la Mfuko wa Hifadhi ya Taifa ya Jamii (NSSF).

Mengi, ambaye kituo chake cha televisheni cha ITV kiliwahi kuendesha mchezo mkubwa wa bahati nasibu ya Jackpot Bingo, pia aliitaja Bahati Nasibu kuwa katika tuhuma hizo, pamoja na mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma.

3 comments:

 1. KWELI KABISA MENGI NA HAWA MAFISADI WENZIE!!WASITUYUMBISHE SISI WAZALENDO!!
  MENGI NA HAWA WAHINDI WOTE LAO MOJA NA NDIO MAANA KILA KUKICHA SASA HIVI KUMEKUA NA MARUMBANO KATI YAKE NA WAFANYABIASHARA WENZIE.
  MENGI AMEKUA NA HISTORIA NDEFU KTK UGOMVI NA WANAOONESHA KUTISHIA MASLAHI YAKE.
  HAKUNA UZALENDO ALIONAO KWA TAIFA NA NDIOMAANA ANAPENDA KUWEKA MASLAHI YAKE MBELE NA KUJILIMBIKIZIA MALI

  ReplyDelete
 2. ANGALIENI UFISADI MPAKA KWENYE VYOMBO VYA HABARI,MENGI AMEKUA AKITUMIA VYOMBO VYAKE KUJITANGAZA NA KULINDA MASLAHI YAKE.
  MAFISADI MENGI NA WAHINDI WANAGOMBA NIA KITOWEO(MNOFU) CHA WATANZANIA MASKINI WENYE NJAA.MUNGU WANGU TUTAKULA WAPI SISI WALALA HOI MAANA MIFISADI HAITOSHEKI TU.
  MENGI ANATUDANGANYA WATANZANIA HOHE HAE KULINDA MASLAHI BINAFSI KWA KUTUMIA UZALENDO HIVI SISI WAZALENDO WA KWELI AMBAO NI MASKINI TUKIAMBIA KEMPISKY INAUZWA TUTAWEZA KWELI KUINUNUA?ZAIDI YA YEYE KUFAIDIKA PEKE YAKE?

  MENGI NA WAHINDI MSITUZINGUE


  Suala la Mengi na Rostamu laibukia bungeni

  WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewataka Watanzania kuwa makini katika matumizi ya vyombo vya habari pamoja na mambo yao, akisema matumizi mabaya yataiingiza nchi katika migogoro.

  Pinda alisema hayo jana wakati kipindi cha maswali ya papo kwa papo cha kila Alhamisi ambacho msimamizi huyo mkuu wa shughuli za serikali Bungeni hukitumia kujibu maswali mbalimbali ya wawakilishi hao wa wananchi.

  Alikuwa akijibu swali la kiongozi wa kambi ya upinzania Bungeni, Hamad Rashidi Mohamed, aliyetaka kujua ni hatua zipi zitachukuliwa kwa mtu anayetumia vyombo vya habari kwa manufaa yake binafsi.  “Mheshimiwa waziri mkuu, naomba kuuliza. Katika kutekeleza sera ya utawala bora, je ni halali kwa mmiliki wa chombo cha habari kutumia chombo chake kwa ajili ya kuwashutumu watu wengine,” aliuliza Rashidi na kutaka kujua msimamo wa serikali.

  Akijibu swali hilo, Pinda alisema jukumu la mtu aliyekashifiwa kupitia vyombo vya habari kuamua cha kufanya ni lake mwenyewe na kwamba anaweza kwenda mahakamani au anaweza kunyamaza na kusamehe.

  Alisema Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo imeshaliona hilo na itachukua hatua stahiki kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa jambo hilo.

  Waziri Mkuu pia alisema suala la mtu kumiliki vyombo vya habari na kutumia vyombo hivyo kwa kuwakashifu watu wengine halipendezi na halitavumiliwa hata kidogo.

  Suala hilo la matumizi mabaya ya vyombo vya habari limetinga Bungeni wakati kukiwa na mjadala mkali juu ya kitendo cha mfanyabiashara Regnald Mengi kutangaza hadharani watu watano aliowatuhumu kuwa ni mafisadi, akiwabatiza jina la 'mafisadi papa' na kuitaka serikali iwachukulie hatua.

  Kitendo cha Mengi, ambaye anamiliki magazeti, television na radio, kimetafsiriwa na aliowatuhumu na watu wengine kuwa ni kutumia vibaya vyombo vyake vya habari, baadhi wakihoji sababu za kutowapa fursa watuhumiwa hao kujibu kama maadili ya uandishi yanavyotaka.

  Tayari watu wawili kati ya watano waliotajwa wamechukua hatua dhidi ya kitendo cha Mengi, baada ya mfanyabiashara Yusuf Manji kufungua kesi akidai fidia ya Sh1 kwa kukashifiwa na Rostam Aziz kutoa saa 24 kwa Mengi ili amsafishe kabla ya kuchukua hatua za kisheria.

  Mjadala huo wa kitendo cha Mengi pia uliendelea nje ya Bunge, baada ya viongozi wa umoja wa vijana wa CCM mkoani Tabora kujitokeza jijini Dar es salaam na kumtaka mfanyabiashara huyo awaombe radhi kwa kumchafua mbunge wao wa jimbo la Igunga, Rostam.

  Nora Damian anaripoti kuwa mwenyekiti wa umoja huo, Robert Kamoga aliwaambia waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) Mengi alipaswa kupeleka ushahidi, kushtaki au kufungua kesi dhidi ya mtu yeyote anayehujumu taifa na si kuwahukumu watu hadharani.

  Alidai kuwa Rostam ni msafi kwa kuwa hajafikishwa kwenye chochote cha sheria na kwamba bado ni mtuhumiwa.

  “Tunaiomba serikali iangilie upya sheria na matumizi haya mabaya ya vyombo vya habari ambayo yanaweza kusababisha mtikisiko mkubwa kwenye nchi,” alisema Kamoga.

  Alidai kuwa kauli za Mengi zinatoa taswira kuwa serikali imeshindwa kutekeleza

  ReplyDelete
 3. hapa bwana kitu kikubwa ambacho nimemona ni kuwa serikali na mafisadi lao ni moja,
  haiwezekani kwa serikali kuwatetea watu ambao ni watuhumiwa wa ufisadi kwa nguvu zote namna hii,
  nadhani na hii ni kutokana na kwamba uchaguzi umekaribia na mafisadi ndio wanaowadhamini hawa waheshimiwa wetu..
  kwa hiyo huu unaoendelea ni mchezo tu wa kuwababaisha watu ili watu washindwe kuelewa nini kinachoendelea...

  ReplyDelete