Saturday, May 30, 2009

Dereva wa Adventure afungwa miaka 150.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida imemhukumu dereva wa magari ya Kampuni ya Adventure ya jijini Mwanza kwenda jela miaka 150 kwa kosa la kusababisha vifo vya watu tisa.

Dereva huyo anafahamika kwa jina la Robert Willson [37] amehukuwa kwenda jela miaka hiyo kwa kupatikana na makosa yapatayo 49 yaliyokuwa yakimkabili Mahakamani hapo.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu wa Mahakama hiyo John Chaba.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo Mwendesha Mashitaka Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Jimmy Gwae alimwomba Hakimu kumpa adhabu kali mshitakiwa kwa kuwa iwe fundisho kwa madereva wengine wazembe wanaopoteza maisha ya abiria bila hatia.

Hakimu Chaba alitoa hukumu hiyo kwa kuridhika na ushahidi uliotolewa na pande zote mbili na upande wa mashitaka kuthibitisha hatia.
Hakimu alimpa adhabu mshitakiwa ya kwenda jela miaka minne kwa kila kosa la kusababisha vifo vya watu tisa wakiwemo watatu waliokufa kwenye lori.
Na katika shtaka la pili lililokuwa na makosa 39 amempa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa.

Na katika kosa lake la tatu la kuendesha gari bila leseni alipe faini ya Sh.30,000/ akishindwa faini basi atakwenda jela miezi sita.

Hivyo katika kila shtaka imepatikana dereva huyo atatumikia kifungo cha kwenda jela miaka 153 na atatumikia kifungo hicho kwa wakati mmoja.

Awali ilidaiwa kuwa Februari 10, mwaka jana, majira ya saa 3 usiku katika barabara ya kuu ya Singida -Dodoma eneo la kijiji cha Puma mshitakiwa alisababisha ajali hiyo.

Ilidaiwa kuwa dereva huyo aliendesha gari aina ya Scania kwa mwendo kasi na baadae kushindwa kulimudu na kuua watu tisa.

Ilidaiwa kuwa dereva huyo alikuwa akiendesha gari hilo kutoka Kigoma kuelekea Dar es Salaam na kugongana uso kwa uso na lori na kusababisha vifo vya watu hao na majeruhi kadhaa na kusababisha ulemavu kwa majeruhi.

No comments:

Post a Comment