Friday, May 29, 2009

Shabiki wa Manchester Aua Wanne Nigeria baada ya timu yake kufungwa na Barca.

Shabiki mmoja wa Manchester United nchini Nigeria ambaye hakukubali matokeo ya timu yake kufungwa jana na Barcelona amewaua kwa kuwagonga na gari washabiki wanne wa Barcelona na kuwajeruhi wengine kadhaa wakati walipokuwa wakishangilia Barcelona kuchukua ubingwa.

Ushabiki wa soka uliopitiliza mipaka barani Afrika umesababisha shabiki mmoja wa Manchester United nchini Nigeria ambaye alishindwa kuvumilia kuona washabiki wa Barcelona wakishangilia kutwaa kombe la mabingwa wa ulaya, kufanya mambo ambayo mtu unaweza usiamini.

Shabiki huyo wa mashetani wekundu aliwaua washabiki wanne wa Barcelona baada ya kuendesha gari lake kwa kasi na kuwagonga washabiki wa Barcelona waliokuwa wamekusanyika kushangilia ushindi wa timu yao.

Tukio hilo lililotokea kwenye mji wa Ogbo nchini humo.

Washabiki wa Barcelona walikuwa wamekusanyika wakishangilia ushindi wakati shabiki huyo wa Manchester alipowavamia na kuwagonga na mini bus yake.

Washabiki wanne wa Barcelona walifariki hapo hapo na wengine 10 walijeruhiwa vibaya.

Taarifa ya polisi wa Nigeria ilisema kwamba shabiki huyo wa Manchester alikuwa akipita zake wakati alipoona kundi la washabiki wa Barcelona waliokuwa wamekusanyika wakishangilia na ndipo alipoamua kuligeuza gari lake na kuliendesha kwa kasi na kuwagonga washabiki hao.

Shabiki huyo amekamatwa na anashikiliwa na polisi nchini humo.Timu kubwa za ulaya zina wapenzi wengi wa soka barani Afrika.
Afrika kuna baadhi ya wapenzi wa timu za ulaya ambao upenzi wao unawazidi hata wanachama na wachezaji wa timu hizo.
Mwanzoni mwa mwezi huu shabiki mmoja wa timu ya Arsenal alijinyonga nchini Kenya baada ya Arsenal kufungwa 3-1 na Manchester kwenye mechi ya nusu fainali.

Suleiman Alphonso Omondi mkazi wa Nairobi alikutwa amekufa akiwa amevaa jezi yake ya Arsenal muda mfupi baada ya mechi kuisha na Arsenal kutupwa nje ya kombe la mabingwa wa ulaya.Timu za Uingereza zinaongoza kwa kuwa na washabiki wengi barani Afrika kuliko timu za nchi zingine za ulaya.

No comments:

Post a Comment