Sunday, May 17, 2009

Walimu Dar kuweka CAMP Ikulu.

CHAMA Cha Walimu Tanzania,CWT kimetishia kuweka kambi Ikulu kwa Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwezi huu, kwa walimu wote wa Mkoa wa Dar es Salaam endapo hawatapatiwa madai na malimbikizo wanayodai kwa muda mrefu.

Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kutoa ahadi ambazo hazitekelezeki kwa walimu kote nchini na wametishia kuweka kambi kwa Kikwete ili kuweza kushinikiza kupatiwa madai yao wanayodai.

Hatua hiyo ilitangazwa jana na Katibu wa Chama hicho, Bw. Ezekiel Oluoch kwenye mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.

Oluoch alisema kuwa ifikapo mwisho wa mwezi huu endapo Serikali kupitia Wizara husika haitaweza kulipa madeni yao, basi watakwenda Ikulu kwa Rais Kikwete ili awatunze hadi hapo watakapopatiwa madai yao.

Alisema kuwa kwa wale walimu ambao wapo mikoani ametoa agizo kwa walimu hao waende kutia kambi kwenye Ofisi za Wakuu wa Wilaya zao hadi hapo watakapolipwa madai yao.

Mbali na kutangaza kuchukua hatua hiyo chama hicho kimechukua uamuzi wa kuishitaki Serikali kwenye Shirika la Kazi Duniani,ILO;Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Pia chama hicho kimeishitaki Serikali kwenye Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Spika wake Samweli Sitta na kwenye Shirikisho la Wafanyakazi ,TUCTA kwa kuwa chama hicho kinaamini taasisi hizo zina uwezo wa kuishinikiza Serikali kulipa madeni hayo kwa wakati.

Alisema madai ya walimu yamekuwa yakishindwa kupatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu na walianza kudai toka mwaka jana lakini majibu yanayotolewa ni urasimu wa Serikali ndio tatizo.

Alisema awali walishakutana na Waziri Mkuu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu lakini hakuna ufumbuzi wa uhakika kuhusu madai hayo na kupelekea walimu kuchoshwa na hali hiyo.

CWT imekuwa kwenye malumbano na mvutano na Serikali kudai madeni yao hadi kufikia hatua ya kugoma nchi nzima, lakini Serikali iliweza kukimbilia Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kuomba kufunga mgomo huo usiendelee.

“Sasa kwa kuwa walishafunga mgomo huo na walimu wakabaki hawana cha kufanya sasa uamuzi watakaouchukua utakuwa ni muafaka” alisema

Kutokana na malalamiko hayo ya mara kwa mara ya walimu, baadhi ya walimu hasa wale wa shahada wameamua kuacha kazi na kukimbilia kwenye shule binafsi kwa kuwa huko wanalipwa mishahara kwa wakati.

No comments:

Post a Comment