Tuesday, May 12, 2009

Wanafunzi wachapwa kwa kuizomea CCM.

WANAFUNZI sita wa Shule ya Sekondari Butundwe-Busanda,wamechapwa viboko sita kila mmoja na kupewa adhabu ya kufyeka huku wengine wakigomea adhabu hiyo baada ya kuuzomea msafara wa mgombea ubunge Jimbo la Busanda kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Pia kutokana na tukio hilo, wazazi wa wanafunzi hao wameandamana hadishuleni hapo kuuona uongozi kwa lengo la kubaini kwa nini watoto waowalifanyiwa kitendo hicho walichokilaani kuwa ni kinyume cha sheria.

Shule hiyo iko katika kijiji alichozaliwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CHADEMA, Bw. Finias Magesa ambaye pia aliwahi kujitolea kujenga mabweni kwa ajili ya wanafunzi hao.

Tukio hilo lilitokea Ijumaa saa 10 jioni wakati msafara wa kampeni za mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Bi. Lolensia Bukwimba ulipopita jirani na shule hiyo na wanafunzi kuzomea huku wakishika vichwani na kuonesha alama ya vidole viwili inayotumiwa na CHADEMA.


Hali hiyo ya kuzomea ilimuudhi mmoja wa makada wa CCM, Bw. Oscar Magoliambaye pia ni mwalimu wa Shule ya Msingi Nyakagomba ambaye alimfuata Mkuu wa shule hiyo Bi. Monica Nzungu.Mara baada ya kuambiwa tukio hilo, Mkuu huyo shule alimwamuru mwalimu mmoja kuwachapa viboko wanafunzi wote, lakini wengine waligoma hivyo kufanikiwa kuwachapa hao ambao wote ni wa kidato cha kwanza.

Baada ya hali hiyo, jana wazazi wa wanafunzi hao waliandamana hadi shuleni hapo na kulazimika kuitisha kikao cha dharura na Mkuu wa shule hiyo ambaye hata hivyo alikana kuagiza mwalimu kuwachapa viboko wanafunzi hao.

Alidai alichosema yeye ni kuwaonya wanafunzi kutoshabikia vyama vyovyote vya siasa, lakini si kuwapiga wanafunzi kama alivyofanya mwalimu huyo ambaye anadaiwa kutoroka tangu siku ya tukio na hajulikani mahali alipo.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa shule alilazimika kuwaomba msamaha wazazi wa wanafunzi hao na kuwa kitendo hicho hakitorudiwa tena kufanywa na mwalimu yeyote shuleni hapo.

Katika hatua nyingine, CHADEMA imemkamata Diwani wa Kata ya Busanda (CCM), Bw. Alphonce Matonange na makada wawili wa chama hicho wakidaiwa kuorodhesha majina na shahada za wapiga kura kwa lengo la kuzinunua.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Busanda, SSP Kimea alisema tayari watu hao wanashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Geita

Alisema mbali ya diwani huyo wengine wanaoshikiliwa ni Bw. Abdallah Ibrahim na Bw. Japhet Shilungule ambao walikutwa wakiwa na orodha ya majina zaidi ya 20 pamoja na namba za shahada za wapiga kura.


"Tunawashikilia watu hao watatu wakati tukiendelea na uchunguzi zaidi juu ya tukio hilo," alisema kamanda huyo na kuongeza kuwa walikamatwa juzi saa 2 usiku.


Source: Majira

No comments:

Post a Comment