Monday, June 22, 2009

Bakili Muluzi anyang'anywa pasipoti

Rais wa zamani wa Malawi Bakili Muluzi amenyang'anywa pasipoti yake na tiketi yake ya ndege wakati akijiandaa kuelekea Uingereza kwaajili ya matibabu kutokana na tuhuma za rushwa zinazomkabili nchini humo.
Bakili Muluzi, alikuwa akijiandaa kusafiri kuelekea Uingereza kwaajili ya uchunguzi wa afya yake wakati maafisa wa kupambana na rushwa walipoamua kumnyang'anya pasipoti yake na tiketi yake ya ndege.
"Tumeishikilia pasipoti ya Muluzi ili kumfanyia uchunguzi wa mambo mbali mbali" alisema Alex Nampota, mkuu wa kitengo cha kupambana na rushwa nchini Malawi (ACB).

Muluzi alikuwa asafiri jana jumapili kuelekea Uingereza ambako amekuwa akienda mara kwa mara kwaajili ya uchunguzi wa afya yake.
Mkuu huyo wa kitengo cha rushwa alifanikiwa kupata kibali toka mahakama kuu cha kushikilia nyaraka za kusafiria za Bakili Muluzi.

Muluzi aliyeiongoza Malawi toka mwaka 1994 hadi 2004 anakabiliwa pia na tuhuma za kuiba dola milioni 12 toka kwenye mfuko wa misaada.

Nampota alisema pia kwamba amefanikiwa kupata kibali cha kuchukua mali za Muluzi na kuzipiga mnada ili kuzirudisha pesa hizo iwapo Muluzi atashindwa katika kesi yake hiyo inayomkabili ambayo bado haijaanza kusikilizwa.

Muluzi ndiye kiongozi wa ngazi ya juu sana kuchukuliwa hatua katika harakati za rais wa Malawi wa sasa Bingu wa Mutharika ambaye amedhamiria kutokomeza rushwa nchini humo.

Muluzi kwa upande wake alisema kuwa ameshangazwa na hatua hiyo ya kumzuia kwenda hospitali kufanyiwa upasuaji ambao hauwezi kufanyika nchini Malawi.

"Sidhani kama nchi hii ingewafanyia marais wake waliopita vitu kama hivi" alisema Bakili Muluzi.
Wakili wa Muluzi, ndugu Jai Banda alisema kuwa wataipinga hatua hiyo ya ACB jumatatu.

No comments:

Post a Comment