Monday, June 22, 2009

Tz yalipa milion 180 alizotafuna mama Mongela-Bunge la Afrika.

Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa, amesema atahoji kuhusu tuhuma zinazomkabili aliyekuwa Rais wa Bunge la Afrika, Balozi Getrude Mongella za matumizi mabaya ya Sh. milioni 180 za bunge hilo wakati wa kujadili ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Fedha za Serikali (CAG).

Wiki iliyopita, aliahidi kulipenyeza suala hilo bungeni ili wabunge waihoji serikali sababu za kumlipia Mongella fedha hizo kama njia ya kumnusuru.

“Hatuoni sababu za kupoteza muda kumzungumzia Mongella ambaye si chochote tena kwa kuwa ameshatoka katika wadhifa huo,” alisema Dk. Slaa alipozungumza na gazeti hili jana.
Alisema kama itabainika katika ripoti ya CAG kuwa serikali ilimlipia fedha hizo mali ya walipa kodi, wataitaka izirejeshe na Mongella aadhibiwe.
Alisema kitu ambacho kinaweza kuwalazimisha kumlipua Mongella bungeni ni kama watabaini kuwa bado anaendelea kuitumia ofisi ya Rais wa Bunge la Afrika.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema hoja kuhusu uhalali wa serikali kulipa Sh. milioni 180 zilizopotezwa na aliyekuwa Rais wa Bunge la Afrika, Balozi Getrude Mongella alipokuwa akishikilia wadhifa huo, haina hadhi ya kujadiliwa kwa vile ni jambo dogo kulinganisha na sababu iliyomfanya aachie ngazi katika Bunge hilo.

Balozi Mongella aliachia nafasi yake katika Bunge hilo Juni 2, mwaka huu na baadaye Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk. Willibrod Slaa alimtuhumu kupoteza fedha hizo, ambazo alisema zimelipwa na serikali.

Membe alisema hayo juzi mjini Dodoma alipozungumza na Nipashe na kuongeza:
“Nenda ukamuulize Mongella akueleze yaliyomsibu Afrika Kusini. Umuulize kwanini aliamua kuachia Urais wa Bunge la Afrika kabla ya muda wake kufika, atakueleza mambo mengi, lakini hiyo ya serikali kumlipia fedha ni ‘kachembe kadogo’ mno.”

Alisema anashauri kuulizwa Mongella kwa vile tuhuma za kumhusisha na upotevu wa fedha hizo, inawezekana zinatokana na wivu au tatizo la utawala au ukaguzi mbovu wa hesabu. Membe alisema pamoja na kwamba, serikali kumlipia madeni Mongella siyo kosa wala dhambi, suala hilo limegubikwa na utata kwani wanaotoa madai hayo hawajafafanua zilikopelekwa fedha hizo kutekeleza malipo hayo.

Alisema Mongella alikuwa Rais wa Bunge la Afrika, hivyo kama kweli serikali imelipa fedha hizo, aliyepaswa kulipwa alitakiwa awe ni Bunge ama Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) au Mongella mwenyewe, jambo ambalo wanaotoa madai hayo hawajaainisha.

Juni 15, mwaka huu, Nipashe ilimkariri Dk. Slaa akisema kwamba, taarifa za uhakika alizonazo zinaonyesha kwamba Balozi Mongella alipoteza kiasi hicho cha fedha ambacho alidai kuwa serikali imekilipa kwa kutumia fedha za walipakodi badala ya kumwajibisha kwa kuisababishia serikali hasara. Dk. Slaa alieleza kushangazwa na kauli ya Mongella kuwaita watu wanaohoji matumizi mabaya ya madaraka aliyofanya kuwa ni wahuni wa kisiasa badala ya kujibu tuhuma zinazoelekezwa kwake kwa kutumia hoja thabiti.

Alisema Mongella anapaswa kutambua kwamba, wananchi wanahitaji kufahamu uadilifu wake alipokuwa akiiwakilisha nchi kwenye chombo hicho cha Afrika na uhalali wake wa kutumia fedha hizo kinyume na taratibu.

Kutokana na hali hiyo, alisema ataipenyeza hoja hiyo bungeni ili chombo hicho kiweze kuihoji serikali na kuongeza kuwa iwapo serikali itashindwa kutoa ufafanuzi wa kina wa jambo hilo, atamshtaki Balozi Mongella, ambaye ni Mbunge wa Ukerewe (CCM) kwa Watanzania ambao fedha zao zimetumika kulipia ubadhirifu huo.

1 comment: