Tuesday, June 23, 2009

Mgodi wa Tulawaka wahofiwa kufungwa.

Kampuni ya Barrick ambayo inaongoza kwa kumiliki migodi kadhaa ya madini nchini imetangaza kufunga mgodi wa dhahabu wa Tulawaka uliopo Biharamulo, mkoani Kagera, wakati wowote kuanzia sasa baada ya dhahabu kumalizika.

Mgodi huo utakuwa wa pili kufungwa kwa madai ya kumalizika dhahabu, baada ya mgodi wa dhahabu wa Buhemba ulioko Wilaya ya Musoma Vijijini, mkoani Mara kufungwa kwa madai kama hayo mwaka juzi.
Mgodi huo ulikuwa ukimilikiwa na Kampuni ya Meremeta.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na mtandao huu, msemaji mkuu wa Kampuni ya Barrick, Teweli Teweli, alisema wameamua kuufunga mgodi huo baada ya kuona kiwango cha madini kimepungua na wameijulisha serikali kuhusu nia yao hiyo.
Alisema kampuni yake imeanza maandalizi ya kuufunga mgodi huo ambao ulianza rasmi uzalishaji mwaka 2005, ambapo waliwekeza kiasi cha dola za Marekani mil. 85 na kutoa ajira kwa watu 239.


“Kiwango cha madini kimepungua katika mgodi huo ndiyo maana tumeanza utaratibu wa kuufunga, tumeshawataarifu wananchi wanaozunguka mgodi huo ambao wamekuwa wakiutegemea waanze kujiandaa,” alisema Teweli.

Aliongeza kuwa moja ya maandalizi waliyoyaanza ni kupanda miti pamoja na kuwaweka wananchi katika hali ya kujitegemea baada ya kuzoea kupata mahitaji yao kutoka kweye mgodi huo.
Kwa mjibu wa mtaalamu mmoja wa miamba ya madini, amebainisha kuwa sheria ya migodi duniani inatamka kuwa maandalizi ya kufunga mgodi lazima yafanyike katika kipindi kisichopungua miaka miwili.

“Mgodi kama ule wa Buhemba wahusika walikiuka taratibu za kimataifa zinazohusu mazingira, sheria zinasema kabla hujafunga mgodi anza maadalizi mapema, ikiwamo kupanda miti na kuvunja mabanda pamoja na kuhamisha mitambo,” alisema mtaalamu huyo.

Mtaalamu huyo aliongeza kuwa kampuni inayoshindwa kufanya hivyo inaweza kushitakiwa au kunyang’anywa vifaa vya uchimbaji madini, kwa kuacha migodi wazi, jambo linaloweza kuleta madhara kwa binadamu na viumbe vingine.
Mpango huo wa Barrick kufunga mgodi wa Tulawaka inasemekana ni sehemu ya maandalizi ya kufungua mgodi wa Buzwagi uliopo mkoani Shinyanga.

Inasemekana kampuni hiyo inasubiri kukamilisha utafiti wa madini ya nikel katika mgodi wa Kabanganiko, Ngara ambao umechukua miongo kadhaa.

Wakati baadhi ya migodi ya madini ikifungwa kwa sababu ya kumalizika madini hayo, takwimu za watu maskini nchini zimezidi kuongezeka kwa kasi.
Taarifa za kufungwa kwa mgodi huo zimekuja huku serikali ikitangaza nia yake ya kufuta misamaha ya kodi ya mafuta kwa kampuni za madini ili kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato.

Hatua hiyo imekuja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuunda kamati iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Mark Bomani, kuchunguza mikataba ya madini na kutoa mapendekezo serikalini kwa ajili ya kuboresha sekta hiyo ambayo kwa muda mrefu inadaiwa kuwanufaisha zaidi wawekezaji.


Kampuni za madini hapa nchini zimekuwa zikishutumiwa kwa kuvuna rasilimali nyingi kuliko kile wanachotoa serikalini kutokana na mikataba mibovu iliyoingiwa na serikali.

No comments:

Post a Comment