Sunday, June 21, 2009

Zaidi ya watu 21 Wafariki Kwa Kunywa na Kuoga Maji yenye sumu -Tarime.

Zaidi ya watu 21 wamekufa huko Wilayani Tarime baada ya kile kinachoaminika kuwa ni kunywa na kuoga maji yenye sumu ya mto Tigithe unaodaiwa kuingiliwa na kemikali za sumu kutoka mgodi wa dhahabu wa North Mara (NMGM).
Watu hao walifariki jana wilayani humo na mifugo kadhaa kudaiwa kupoteza maisha kutokana na sumu hiyo.

Habari za kuaminika kutoka kwa Diwani wa Kata hiyo Bw.Joseph Maya amesema kuwa kati ya hao kuna wanawake watatu ambao mimba zao zimeharibika baada ya kunywa na kuoga maji ya mto huo.
Alisema kuwa kabla ya kufariki dunia kwa watu hao walianza kuwashwa sehemu za mwili, kusokotwa na matumbo, kuharisha, kuhara damu na kutapika na mwisho kufariki dunia.

Ameongeza kuwa, mbali na vifo hivyo katika kata hiyo na kata nyingine za jirani wakazi wa maeneo hayo wamekabiliwa na madhara ya kuchubuka ngozi na baadhi ya mimea iliyo kandokando ya mto huo kukauka kutokana na maji hayo yenye sumu kutiririka kutoka kwenye mgodi huo.

Hata hivyo uongozi wa Barrick Gold ulipoulizwa kuhusiana na vifo hivyo vya wanakijiji wamekiri kuwa ni kweli tindikali zilikuwa zikitiririka kwenye mgodi huo na mgodi huo unachukua hatua za kuzuia jambo hilo lisitokee tena.

Barrick Gold walisema kuwa awali waliweza kuzuia tindikali kuvuja lakini kuna wizi ulifanyika wa kapeti za plastiki zilizokuwa zinazuia maji ya sumu kupenya na kwenda kwenye mabwawa na mito.

No comments:

Post a Comment