Tuesday, June 16, 2009

Chenge awa mtemi wa wasukuma.

MBUNGE wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ambaye amekuwa akiandamwa na kashfa mbalimbali, ametawazwa kuwa mtemi wa kabila la Wasukuma-Bagole, Kanda ya Itilima, wilayani Bariadi.
Chenge alichaguliwa katika sherehe maarufu za kabila hilo, maarufu kama Bolabo, mwishoni mwa wiki, wilayani hapa, ambazo mbali na viongozi wa kimila, Mkuu wa Mkoa, Abbas Kandoro, alikuwa ni miongoni mwa waliohudhuria.
Baadhi ya watu waliokuwepo kwenye sherehe hizo, waliuelezea utemi wa Chenge kwa mtazamo tofauti, huku baadhi wakidai kaupata ili kuweka mambo yake sawa, na wengine wakidai anastahili kupata nafasi hiyo kwa kuwa ni miongoni mwa watu wa kabila hilo.

Mbunge huyo ambaye alilazimika kujiuzulu nafasi yake ya uwaziri alisema, utemi huo ni karama aliyopewa na Mungu na kwamba wajibu huo ni sawa na daraja la kuunganisha jamii ya kabila husika.
"Utemi niliopewa naweza kusema ni karama iliyotoka kwa Mwenyezi Mungu! Kazi hii ya utemi ni nzito kwa sababu ina masuala yake yanayohusiana na mambo ya kimila pamoja na kuunganisha jamii ya kabila husika," alisema Chenge.

Sherehe hizo za kabila la Kisukuma, zilihudhuriwa na watu maarufu akiwemo Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Mshauri wa Watemi, Jaji Michael Bomani, Mwenyekiti wa Watemi wa Wasukuma, Kanda ya Mwanza, Charles Kafipa, mmoja wa washauri wa Watemi Bujora, Jaji Thomas Mihayo, na viongozi watemi wengine kutoka mkoani Shinyanga.

No comments:

Post a Comment