Tuesday, June 30, 2009

JK amedidimiza Uchumi: World Bank.

BENKI ya Dunia (WB) imeeleza kuwa, pamoja na viongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, kuelekeza juhudi zao za kuzifanyia mabadiliko ajenda mbalimbali za uchumi wa nchi, takwimu za mashirika mbalimbali ya kimataifa zimebainisha kuwa, kwa miaka ya hivi karibuni, Tanzania inaendelea kudidimia mwaka hadi mwaka.

Taasisi hiyo kubwa ya kifedha duniani ikiyanukuu mashirika ya Public Expenditure and Financial Accountability, Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uwazi katika matumizi ya fedha za umma pamoja na Transparency International, imebainisha kuwa vigezo vya gharama za kufanya biashara na ushindani wa biashara ya kimataifa viko chini.

Mkurugenzi wa WB Kanda ya Afrika katika nchi za Tanzania, Uganda na Burundi, John Murray Mclintire, alibainisha hayo jana, jijini Dar es Salaam wakati akitangaza miradi ambayo serikali itasaidia kupitia sera ya kuisaidia bajeti.
Miradi ambayo itasaidiwa na benki hiyo ni pamoja na dola milioni 190 kwa ajili ya kupunguza umaskini, dola milioni 220 kwa ajili ya kuisaidia Programu ya Usalama wa Chakula (AFSP), dola milioni 90, kwa ajili ya programu ya kuinua kilimo pamoja na dola nyingine milioni 151 kwa ajili ya upanuzi wa mradi wa huduma za mawasiliano kwa nchi za Malawi, Tanzania na Msumbiji.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, sera ya mabadiliko ya kisheria na serikali za mitaa katika sekta za maendeleo za serikali na binafsi zimeonyesha ufanisi mdogo.
‘‘Ufanisi katika kiashirio cha kifedha umeshuka kutoka dola za Marekani milioni 200 hadi 190, hiki ni kielelezo kuwa hakuna mafanikio ya kisera zaidi yakiwa ni mazingira ya kufanya biashara kwa wazawa na wawekezaji kutoka nje na sera ya mabadiliko katika usimamizi wa fedha za umma,” alisema mkurugenzi huyo.

Iliendelea kuelezwa kuwa, pamoja na ripoti ya mwaka 2008 ya upitiaji wa sera za nchi pamoja na ule wa kitaasisi kuonyesha kuwa Tanzania ilikuwa juu kwa asilimia 3.8, mwaka huu imeonyesha kushuka kwa asilimia 0.9.

‘‘Japokuwa uongozi wa nchi umeonyesha juhudi zake katika kuzifanyia ajenda mbalimabali marekebisho kwa ajili ya kujenga uchumi wa kisasa, utekelezaji wa marekebisho hayo kimfumo umekuwa ukidhoofika kwa miaka kadhaa sasa na kwa baadhi ya maeneo imeonekana kushindwa kufanya kazi kabisa,” aliongeza.

Bila kuitaja awamu ya tatu iliyoongozwa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, Mkuu huyo wa WB alieleza kuwa, Tanzania imetekeleza marekebisho kadhaa na yameonyesha ufanisi mkubwa, hasa katika sera ya uchumi mkubwa (Macro economy) hali iliyothibitishwa na ukuaji wa kuridhisha wa uchumi na kupunguza kabisa mfumuko wa bei.

Aliendelea kueleza kuwa, ukuaji wa uchumi umeendelea kukua kwa kiasi cha asilimia saba kwa miaka mitatu sasa, hali inayoonyesha kuwa kuna ufanisi katika hifadhi ya fedha za kigeni.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa, utafiti wa bajeti ya kaya, ndoto ya kufikia Malengo ya Milenia (MDGs), hapo 2025 imeonyesha hayatafikiwa hata katika maeneo ambayo awali yalionekana yangefikiwa na hata kuondoa umasikini na kupata huduma za afya na majisafi, na kushauri msisitizo katika maeneo hayo unatakiwa.

No comments:

Post a Comment