Tuesday, June 9, 2009

wakutwa wamekufa ndani ya hoteli Dar.

Wahindi wawili,mmoja raia wa Canada na mwingine raia wa Afrika Kusini wamekutwa wamefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha ndani ya vyumba vya hoteli ya Harbours View iliyopo kwenye jengo la JM Mall Jijini.Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Seleiman Kova, ameiambia Alasiri leo asubuhi kuwa miili ya wahindi hao ilikutwa katika vyumba tofauti vya hoteli hiyo, majira ya saa 8:00.

Kamanda Kova amesema kuwa Polisi walipata taarifa toka kwa Meneja Masoko wa hoteli hiyo aitwaye Bw. Laizer Manukwa, aliyeeleza kuwa usiku, kuna mteja wao aliyekuwa chumba namba 10-12, aliyefahamika kwa jina la Sulman Zuber, 41, Mhindi raia wa Canada, alikutwa akiwa amekufa chumbani humo.

Kamanda Kova akasema kuwa katika tukio jingine lililojiri hotelini hapo, ilibainika kuwa katika chumba 12- 09, ghorofa ya pili, mtu aitwaye Nickel Kumar Taluar, 33, raia wa India, alieleza kuwa mpangaji mwenzie ambaye pia ni mhindi aitwaye Yusuf Seda, raia wa Afrika Kusini, alikutwa amekufa pia chumbani kwake.

Aidha, Kamanda Kova akasema kuwa vifo vya watu hao wanaodaiwa kuwepo hotelini tangu Mei 19 mwaka huu havionyeshi kuwepo na purukushani yoyote kabla ya kutokea kwake.

Hata hivyo, akasema taarifa za awali toka kwa uongozi wa hoteli hiyo zinaonyesha kuwa watu hao walirejea jana alfajiri toka kwenye sehemu za starehe na kwamba kuna wakati, mwingine alionekana kwenye maeneo ya Casino ya hotelini hapo.

Akasema inawezekana walikuwa wamezidisha vinywaji walipokuwa katika maeneo hayo.
Akasema kutokana na tukio hilo, Polisi wameunda timu ya wataalam mbalimbali akiwemo Mkemia Mkuu na Daktari ili kuweza kubaini chanzo cha vifo vya watu hao.

Akasema upelelezi unaendelea na hadi sasa hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

No comments:

Post a Comment