Wednesday, July 8, 2009

Askofu adai mafisadi wanauhofia waraka wa Kanisa Katoliki

Askofu msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Methodius Kilaini amesema mafisadi wanauhofia mwongozo uliotolewa na kanisa hilo ambao unaweka vipaumbele vya nchi katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, ndiyo maana wanaupinga.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya misa ya upadrisho iliyofanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam, Kilaini alisema mwongozo huo ulianza kutumika tangu uchaguzi wa mwaka 1995 na kusisitiza kuwa kwa mwaka huu watu wengi wameshtuka kutokana na masuala ya ufisadi.

Kanisa hilo lilitoa vitabu viwili vya mwongozo na vipaumbele vya nchi kabla ya kuuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, mwongozo ambao umekumbana na vipingamizi kutoka kwa baadhi ya wanasiasa kwa madai kuwa dini inaingilia mambo ya siasa.

“Kwanza napenda watu waelewe kuwa mwongozo hauna lolote kuhusu dini kama watu wanavyodhani, kwa sasa jamii imeshtuka kuhusu vitendo vya rushwa na ndiyo sababu baadhi ya wanasiasa wanapinga mwongozo huo kwa kuwa unalenga kuwafungua watu macho na kukemea vitendo vya ufisadi,” alisema Kilaini.

“Ninachowataka wanasiasa wote washiriki ni kupiga vita ufisadi. Asiyetaka kupigana na ufisadi tusimchague, na ndivyo mwongozo huo unavyosema,” alisema.

Alifafanua kuwa mwongozo huo unazungumzia juu ya serikali na msimamo wake na wala si kumchagua mtu fulani wala chama fulani kwa ajili ya kumpa uongozi.

Alisema kama kutakuwa na kiongozi wa dini au mtu yeyote wa dini atakayezungumzia masuala ya kumchagua mtu ama chama fulani cha siasa, atakuwa amepotoka na kwamba huo ndio msimamo uliomo kwenye mwongozo huo.

“Watu wausome mwongozo huo kwa moyo mweupe na ninaamini wataufurahia, utakuza ufahamu juu ya masuala ya kidemokrasia,” alisema Kilaini.

Kauli ya Kilaini imetolewa wakati ambapo baadhi ya wabunge wamejitokeza kuitahadharisha serikali kuhusu mwongozo huo kwenye mkutano unaoendelea wa Bunge la Muungano, wakidai kuwa ukiachwa nchi inaweza kuingia kwenye matatizo ya udini.

Mbunge wa Kigoma Kusini, Manju Msambya aliushutumu mwongozo huo aliouita kuwa ni "waraka wa Kiaskofu" wakati akichangia hotuba ya makadirio na matumizi ya Wizara ya Sheria na Katiba, akisema unawafundisha waumini wake kuhusu namna ya kuchagua viongozi kwa imani zao na kuonya kuwa nchi inaweza kuingia kwenye vurugu.

Msambya ambaye hakutaja moja kwa moja dhehebu la dini lililotoa waraka huo, alisema unapingana na kanuni kwamba watu wasichanganye dini na siasa.

Akizungumza kwa jazba, Msambya, ambaye katika mchango wake alitaka tamko la serikali kuhusu sababu za nchi kutojiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) na kutoundwa kwa Mahakama ya Kadhi, alisema alichukizwa na kitendo cha waziri ambaye hakumtaja jina, kwamba alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusiana na waraka huo, aliusifu akisema ni mzuri kwa sababu ni moja ya elimu ya kupiga kura.

Lakini Askofu Kilaini alisema mwongozo huo haukutungwa na maaskofu wala mapadri wa kanisa hilo na kufafanua kuwa umetungwa na Chama cha Wataalamu wa Kanisa Katoliki (CPT) na kwamba wao waliupa baraka zote baada ya kuusoma na kuona unafaa.

Kabla ya kuongea na waandishi wa habari, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliwapa daraja la upadri, mashemasi watatu.
Mashemasi hao ni pamoja na Joseph Mkonde, Joseph Mapunda ambao watakuwa mapadri wa jimbo, huku Hendrick Mambwe akienda kulitumikia kanisa hilo nchini Ethiopia.

3 comments:

  1. Watu wa kanisa wapo mstari wa mbele na mambo ya siasa! Shughuli ipo...

    ReplyDelete
  2. Dini na siasa vimechanganywa hapo, ila dini fulani wakivitaja vipaumbele vyao ndo udini unaonekana ila wao sio wadini. Ndo maana hatupati maendeleo kutokana na huu udini, hasa hawa wakatoliki ni wadini sana ndo maana hatukumchagua Slaa!!

    ReplyDelete
  3. Hatuja-mchagua kabisaa mwanaharamu Slaa.

    ReplyDelete