Saturday, July 4, 2009

Ferguson amnasa Owen!

Kocha wa Manchester United Alex Ferguson amefanya usajili ambao umewaacha watu wengi wakijiuliza maswali mengi baada ya kumsajili mshambuliaji wa Newcastle Michael Owen ambaye watu wengi wanafikiria kuwa kiwango chake cha soka kimeisha.
Usajili wa Michael Owen kuhamia Manchester United uliwashtua watu wengi hata Michael Owen mwenyewe alikiri kwamba hakuwa na mawazo ya kusajiliwa na Manchester.
"Nilikuwa kwenye mazungumzo na klabu mbali mbali wakati Alex Ferguson aliponipigia simu bila kutegemea siku ya jumatano na kuniambia kwamba anataka tunywe chai pamoja asubuhi ya alhamisi na tulipokutana ndipo aliponiambia kuwa anataka kunisajili Manchester, bila hata kufikiria nilimkubalia hapo hapo" alisema Owen.

"Hii ni bahati kubwa sana kwangu na nimeipokea kwa mikono yote miwili" alisema Owen.

Mkataba wa Michael Owen na Newcastle United ambayo imeshuka daraja msimu uliopita, ulimalizika wiki hii na kumfanya Michael Owen ahamie bure Manchester kwa mkataba wa miaka miwili akilipwa kutokana na mechi atakazokuwa akicheza.
Alex Ferguson ana imani kuwa Owen atasaidia kuimarisha safu yake ya ushambuliaji baada ya kuondoka kwa Cristiano Ronaldo huku Carlos Tevez naye akisisitiza nia yake ya kuondoka.

"Owen ni mmoja wa washambuliaji wakubwa sana duniani na rekodi yake ya kufunga magoli hakuna mtu atakayeitilia shaka" alisema Alex Ferguson.

Owen sasa ana kazi ya kugombania namba ya kudumu katika safu ya ushambuliaji ya Manchester wakati huo huo akijaribu kuonyesha kiwango kitakachomshawishi kocha wa timu ya taifa ya Uingereza, Fabio Capello amuite kwenye kikosi chake kitakachoshiriki kombe la dunia mwakani nchini Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment