Wednesday, July 22, 2009

Mchungaji anaswa na viungo vya Albino

MCHUNGAJI wa Kanisa la Baptist wilayani Magu, Bw. Alfred Komanya (35), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na viungo vya albino, aliyeuawa Juni 26 mwaka huu eneo la Ibanda Relini, jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Bw. Jamal Rwambow, polisi walifanikiwa kumkamata mchungaji huyo na watu wengine kadhaa wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji albino huyo, Bw. Aron Nongo .
Kamanda Rwambow aliwataja watuhumiwa wengine wanaoshikiliwa kuwa ni Bw. Chacha Mwita (30) mkazi wa Mahina, Bw. Mathew Mlimi (21), mkazi wa Mahina Nyangulukulu, Bw. Alex Joseph (24) mkulima na mkazi wa Mahina, na Bw. Kishosha Komanya (60), mganga wa jadi mkazi wa Mahina.
Wengine ni Bw. Pascal Mashiku (28) mkazi wa maeneo ya Semba, Buhongwa, Bw. Gervas Komanya (58) ambaye ni mganga wa jadi mkazi wa Nyanguge wilayani Magu na Bw. Paulo Genji (36) mkazi wa Kishiri, Kanindo jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa Kamanda Rwambow, baadhi ya watuhumiwa, katika mahojiano yao na Polisi, walikiri kuhusika moja kwa moja na mauaji hayo na kudai kuwa kabla ya kufanya unyama huo, walikwenda kwa waganga wa jadi ili kupewa dawa za kufanya mauaji hayo bila kukamatwa na mkono wa dola.
Kamanda Rwambow, alisema Jeshi la Polisi litatoa zawadi ya sh. milioni moja kwa raia wema waliotoa taarifa na baadaye kufanikisha kukamatwa watuhumiwa.

No comments:

Post a Comment