Tuesday, July 21, 2009

wizi kwenye ATM-WEZI WATUMIA KIFAA KUNASA NAMBA ZA SIRI KIRAHISI

Wimbi la wizi wa fedha kwenye akaunti za wateja kupitia mashine za ATM sasa umefikia kiwango cha kutisha baada ya polisi kukamata watu wawili raia wa Bulgaria waliokuwa wanatumia chombo maalumu kunasa namba za siri za kadi na kuchota fedha kirahisi.

Jeshi la Polisi, Kanda ya Dar es Salaam limesema watu hao wanatuhumiwa kuchota kiasi cha Sh70 milioni kutoka kwenye akaunti za wateja wa benki mbalimbali ambao huchukua fedha zao kwenye mashine hizo za ATM.
Kwa mujibu wa polisi, kifaa hicho kina uwezo wa kunakili taarifa za kadi za ATM, ikiwa ni pamoja na namba za siri ambazo huwawezesha wezi kuingia kwenye mashine na kuchota kiasi cha juu cha fedha kulingana na kiwango cha ukomo wa mashine hizo.


Kamanda wa Polisi wa Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana kuwa, kukamatwa kwa raia hao wawili wa Bulgaria kulitokana na jeshi lake kuweka mtego baada ya kupata taarifa kuwa kuna watu wanaojihusisha na wizi wa fedha za wateja kwenye ATM kwa kutumia kifaa hicho.

Kamanda Kova alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na uongozi wa benki ya Barclays iliyo wilayani Kinondoni waliwakamata watu hao wawili, Nedko Stanchen, 34, na Stella Nedekcheva, 23, wote raia wa Bulgaria.

“Tumefanikiwa kuwakamata baada ya kuweka mtego katika ATM. tulimweka mfanyakazi wa benki hiyo kwa siri aliyekuwa anafanya usafi (kwenye ATM) ndipo alipogundua kuwekwa kwa kifaa hicho katika mashine,” alisema Kamanda Kova.

Kamanda Kova alisema watuhumiwa hao walikuwa wanazunguka kwenye mashine mbalimbali za ATM na kuweka kifaa hicho ambacho hurekodi namba za siri za kuingilia kwenye akaunti ya mteja na baadaye kuchota fedha.

Alisema kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakiingia kwenye ATM mara wanapoona mteja ametoka na hivyo kuwa rahisi kwa kifaa chao kunakili taarifa za kadi ya mteja huyo.

Alisema inasadikiwa kuwa watuhumiwa hao wameshaiba kiasi cha Sh70 milioni kupitia mashine za benki mbalimbali na baada ya kupekuliwa walikutwa na kadi tano za ATM za benki ya Barclays na Stanbic pamoja na vifaa vya aina mbalimbali wanavyohisi vinatumika kwenye wizi huo.
Kwa mujibu wa tovuti ya snopes.com inayozungumzia uhalifu wa aina hiyo kwenye mashine za fedha, kifaa hicho hubandikwa kwenye ATM na kuonekana kuwa sehemu ya mashine kutokana na umbile lake, lakini kazi yake kubwa huwa ni kuchukua namba ya kadi ya ATM na namba za siri.
Wezi hao pia huficha chombo kingine kidogo pembeni ya mashine hiyo ya ATM ambacho huonekana kama ni cha kuhifadhia matangazo ya benki husika. Chombo hicho hufanya kazi ya kuchukua picha za vidole wakati mteja akiingiza namba zake za siri.


Picha hizo hurushwa moja kwa moja hadi kwa wezi ambao huwa umbali wa mita zisizozidi 200, hasa nyakati za jioni na baadaye kwenda kwenye mashine hiyo na kuchukua fedha kutoka kwenye akaunti mbalimbali kwa muda mfupi sana.

Njia zingine ambazo hutumiwa na wezi kwenye mashine za ATM ni ile inayojulikana kama 'Lebanese loop'. Kwa mujibu wa tovuti mbalimbali, wezi huchomeka kadi ya plastiki juu ya tundu la kuingizia kadi ya ATM na hivyo kuifanya ishindwe kusoma.

Inaposhindwa kusoma, kwa mujibu wa tovuti hiyo, mashine hutoa maneno yanayotaka uingize tena namba za siri, hali ambayo humfanya mwizi anayekuwa nyuma ya mteja, kukariri kirahisi namba za siri na kuitumia kadi ya mteja mara anapoondoka kwa kudhani kuwa kadi yake imenasa.
Kamanda Kova hakutaka kutoa maelezo zaidi kuhusu mintaarafu ya watu hao.
Kova aliwataka wateja wanaotumia kadi za ATM kujiwekea utaratibu wa kuangalia salio mara kwa mara kujua usalama wa fedha zao kwani kuna mbinu za wizi.


Alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani hivi karibuni baada ya uchunguzi kukamilika.

Wakati huo huo, jeshi la polisi limefanikiwa kuzuia wizi kwenye kiwanda cha Alfa Krust Ltd, baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema na kumkamata mtu anayetuhumiwa kutumia funguo bandia kuingia kwenye ofisi mbalimbali.

Kamanda Kova alisema mtuhumiwa huyo, Habibu Seif alikutwa na funguo 21 zenye uwezo wa kufungua milango yote ya kiwanda hicho hadi chumba cha mkurugenzi.

No comments:

Post a Comment