Thursday, July 23, 2009

spika wa bunge na matumizi makubwa ya fedha za walala hoi.

Mwenendo wa kimaisha na kimadaraka wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta, umekuwa ukifuatiliwa kwa karibu na watu mbalimbali ndani ya Bunge na nje;
Tanzania Daima Jumatano imebaini. Taarifa za uhakika ambazo Tanzania Daima Jumatano imezipata kutoka vyanzo vya kuaminika serikalini na bungeni zinaeleza kwamba, kufuatiliwa huko kwa Sitta, kunachangiwa kwa kiwango kikubwa na hatua yake ya kutangaza kujitoa mhanga, kupambana na vitendo vya ufisadi miongoni mwa viongozi wa dola.

Vyanzo vya kuaminika vilivyozungumza na gazeti hili, vimedokeza kwamba, hatua ya kuanza kufuatiliwa kwa karibu kwa Sitta inatokana na kuvujishwa kwa taarifa ambazo zinaihusisha ofisi ya kiongozi huyo wa juu bungeni na matumizi makubwa ya fedha za umma kwa mambo yanayotafsiriwa kuwa ni ya anasa na yasiyo na msingi.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, sababu kubwa inayochochea kufuatiliwa kwa mwenendo wa matumizi ya ofisi ya Spika, kumechagizwa na kuwapo kwa taarifa za Bunge kukabiliwa na hali ya ukata mkubwa kifedha zilizothibitishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Huduma za Bunge, Mbunge wa Bumbuli, William Shellukindo (CCM).

Moja ya eneo lililoibua maswali mengi kuhusu matumizi ya fedha katika ofisi hiyo, ni ile inayohusishwa na hatua yake ya kuamua kumpangishia Spika Sitta nyumba binafsi kwa gharama za dola za Marekani 8,000 kwa mwezi (zaidi ya shilingi milioni 10).

Katika hili, kikubwa kilichoibua maswali ni hatua ya ofisi hiyo ya Bunge kuamua kumhamisha kutoka katika nyumba ya awali aliyopewa na serikali kwa maelezo kwamba, haikuwa na hadhi inayolingana na wadhifa wa u-Spika ambao miezi kadhaa iliyopita Sitta mwenyewe alipata kuufananisha kimamlaka na ule wa uwaziri mkuu serikalini.

Mbali ya kodi hiyo ya pango, kingine kilichoibua maswali na taarifa zake kupenyezwa nje ya ofisi hizo za Bunge, ni hatua ya kutumia zaidi ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya kununulia samani katika nyumba hiyo mpya ya Spika ambayo tayari ameshahamia. Kama hiyo haitoshi, taarifa zaidi ambazo Tanzania Daima Jumatano inazo ni zile zinazohoji kuhusu fununu za Ofisi ya Bunge kuagiza gari jipya aina ya Mercedes Benz ambalo litakuwa likitumiwa na Spika likikadiriwa kununuliwa kwa shilingi milioni 300, huku tayari kiasi cha shilingi milioni 270 zikiwa zimeshalipwa.

Hata hivyo, wakati taarifa hizo zikivujishwa kwa malengo ambayo Tanzania Daima Jumatano haliwezi kuyabainisha japo kwa sasa, Shellukindo amejitokeza na kumtetea Spika na ofisi yake kwa maamuzi yote yaliyofanywa na ofisi yake.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu kutoka Dodoma jana, Shellukindo alisema maamuzi yote yaliyofikiwa na Ofisi ya Bunge kuhusu mafao anayostahili Spika yalifanyika baada ya kupata baraka zote za Rais Jakaya Kikwete.

Shellukindo ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya Huduma za Bunge, alitoa kauli hiyo baada ya kutakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu madai ya tume yake kuidhinisha malipo makubwa kwa ajili ya kodi ya pango ya nyumba anayoishi Spika.
Katika majibu yake, Shellukindo alisema maneno yanayosambazwa sasa kuwa Bunge linatumia fedha nyingi kwa ajili ya kulipa kodi ya pango ya nyumba ya Spika, hayana msingi kwa sababu malipo hayo yameidhinishwa na Rais Kikwete.

Alisema, ingawa kwa sasa Bunge lina hali mbaya kifedha, ukata huo hausababishwi kwa namna yoyote na ukubwa wa malipo bali ni ukweli kwamba sehemu zote sasa zinakabiliwa na tatizo hilo.

“Spika ana stahili zake kama Spika, hivyo kulipiwa kodi ya pango kwa dola 8,000 kwa mwezi na samani zake za ndani kugharimu zaidi ya sh mil 200 si jambo la ajabu. Ni kiongozi mwenye hadhi hiyo. Rais anajua, ndiye anayeidhinisha stahili zote za Spika.
Hivyo hakuna jambo la ajabu hapo,” alisema Shellukindo. Akizungumza kuhusu Spika kuishi nyumba ya kupanga badala ya ile aliyopewa na serikali, alisema hilo lilitokana na ukweli kwamba nyumba iliyopewa awali haikuwa ya hadhi yake, hivyo ilibidi atafutiwe nyingine ya kupanga kutoka kwa mtu binafsi.

“Kila kitu anachopata Spika sasa, ndiyo walichokuwa wakipata waliomtangulia katika wadhifa huo. Bunge hatuna nyumba ya Spika, sasa ile ya serikali haikuwa na hadhi ya Spika kwa kweli. Ikabidi atafute ya kupanga kwa watu binafsi. “Hili tumeliona kuwa ni tatizo na sasa Bunge lina mpango wa kujenga nyumba ya Spika. Nyumba hiyo haitakuwa ya Spika Sitta, bali maspika wetu watakaokuwa wakichaguliwa ndio watakuwa wakikaa humo,” alisema.

Shellukindo aligusia pia suala la baadhi ya watumishi wa taasisi hiyo kutokuwa na sifa na kueleza kuwa, jambo hilo linaweza kuwa chanzo cha matatizo ya kifedha yaliyolikumba Bunge kwa sasa. Alisema, tume yake inazo taarifa kuwa Mhasibu Mkuu wa Bunge (jina tunalihifadhi) amekuwa akionekana hawezi kuendelea kuwa mtumishi wa Bunge kwa wadhifa huo kwa sababu ya kuwa na kiwango kidogo cha elimu.

“Haiwezekani yeye awe analipa tu, tumempa muda wa kusoma ili awe na sifa za uhasibu. Kwa sasa hana sifa zinazokubalika kuendesha taasisi kama Bunge. Yeye ana vyeti vya chini chini, lakini mhasibu anatakiwa kuwa na CPA,” alisema Shellukindo.

Alisitiza kuwa upo uwezekano wa mahesabu katika taasisi hiyo kuwa ni yenye utata kutokana na udhaifu wa mhasibu huyo. Hata hivyo alisema, awali kabla ya kufanyika kwa mabadiliko ya sasa hivi, tume yake ilikuwa haina uwezo wa kuchukua hatua zozote za kikazi kwa mhasibu huyo kwa sababu Idara ya Uhasibu ya Bunge ilikuwa ikiripoti moja kwa moja Hazina.
Alieleza zaidi kuwa hivi sasa tume yake imepewa meno na iko kwenye mkakati wa kuhahakisha kila senti ya Bunge inafahamika ilivyotumika kwa vile wahasibu wote sasa wanaripoti katika tume hiyo baada ya kufanyika mabadiliko katika muundo wa utumishi kwa wafanyakazi wa Bunge.
Shellukindo alisema kwa kuanza, tume yake imepanga kuanza kupokea ripoti za Idara ya Uhasibu ya Bunge kila baada ya miezi mitatu ili kudhibiti ufujaji wa fedha wa aina yoyote katika taasisi hiyo.

No comments:

Post a Comment