Monday, July 20, 2009

Nchi inatikisika kwa uongozi dhaifu- Lipumba

Matatizo yanayoitikisa Tanzania na kutishia mgawanyiko mkubwa miongoni mwa jamii kwa misingi ya ukabila na udini ni matokeo ya uongozi dhaifu usiokuwa na majibu kwa wakati muafaka.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alipokuwa akihutubia Mkutano wa Hadhara wa chama hicho katika Kata ya Mwananyamala.
Prof. Lipumba alidai kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete imeonesha udhaifu katika kuyatolea ufafanuzi na maamuzi masuala makubwa yanayoitatiza nchi na kutishia mgawanyiko miongoni mwa Watanzania.
Aliyataja baadhi ya masuala yanayoitikisa nchi kwa sasa kuwa ni pamoja na Mahakama ya Kadhi, Tanzania kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislam (OIC), ufisadi miongoni mwa viongozi nchini na kuongezeka umaskini miongoni mwa Watanzania.

"Ndugu zangu nawaambia yote mnayoyaona yakitokea sasa ni matokeo ya serikali dhaifu inayoongozwa na Kikwete (Rais Kikwete) mliyemchagua 2005, ni hatari sana kuchagua kiongozi dhaifu, legelege ambaye hawezi kusimama na kukemea maovu au mambo hatari yanayotishia uhai wa taifa," alisema Prof. Lipumba.

Prof. Lipumba huku akifafanua dhamira ya CUF kuwazindua wananchi kupitia 'Operesheni Zinduka' ili wananchi wazinduke na kuona udhaifu na ufisadi wa viongzi wao, alisema umasikini wa Watanzania unazidi kuongezeka huku viongozi wakizidi kujineemesha kwa kula rushwa na kupora rasilimali za nchi.

"Ripoti ya Serikali iliyotolewa mwaka jana ilionesha kuwa idadi ya masikini wa kutupwa imeongezeka kutoka milioni 11.4 mwaka 2001, hadi milioni 12.9 mwaka 2007, hii maana yake ni kwamba masikini wameongezeka kwa milioni 1.5 sasa haya ndiyo Maisha Bora kwa Mtanzania mliyoahidiwa na CCM?," alihoji.

Akizungumzia suala la Mahakama ya Kadhi, Prof. Lipumba, alisema kuwa Rais Kikwete alipaswa kuwa amelitolea ufafanuzi na uamuzi wa suala hilo ambalo liko katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 ambayo ndiyo iliyotumika kumwingiza madarakani.

"Katika Ilani hiyo sura ya 8, ibara ya 108 b, CCM iliahidi kuhakikisha kuwa tatizo la kukosekana kwa Mahakama ya Kadhi, linatafutiwa ufumbuzi lakini sasa hivi cha ajabu wanawaambia waislam waunde Mahakama hiyo wao wenyewe, nje ya Serikali, sasa wakiunda mahakama kama za Somalia itakuwaje?," alihoji tena Prof. Lipumba.

Prof. Lipumba alisema kuwa katika hilo, Rais Kikwete alitakiwa kumuuliza Rais wa Kenya, Bw. Mwai Kibaki, alipotembelea juzi nchini kwani nchi hiyo ina Mahakama ya Kadhi na wala haina tatizo lolote.
Alisema kuwa kwa kipindi cha miaka minne madarakani serikali ya CCM chini ya Rais Kikwete imeshindwa kutumia fursa ya kijiografia ambayo Tanzania imebarikiwa kuwa na bahari, maziwa makuu, mito mikubwa na madini mbalimbali.

"Mwaka jana Tanzania imesafirisha dhahabu yenye thamani ya dola milioni 800, lakini Serikali iliambulia dola milioni 24 tu na zingine zote zimepotea kwa misingi ya kifisadi na mikataba mibovu,"

Alidai kuwa katika kesi za ufisadi Rais mstaafu, Benjamin Mkapa anapaswa kuwa namba moja kwa sababu aliruhusu ukwapuaji mkubwa wa rasilimali za nchi hii hasa katika awamu yake ya mwisho ya utawala.

Alisema aliposhutumiwa juu ya hilo baadhi ya viongozi waliwataka wanaomtuhumu watoe ushahidi. Alidai kuwa sasa ushahidi umepatikana tena kutoka kwa Taasisi ya Kuchunguza Ufisadi ya Uingereza (SFO) ukiwahusisha baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali na ufisadi wa rada.

"Katika ufisadi wa rada wataalam walishauri Serikali inunue rada yenye thamani ya dola milioni 5, lakini wao wakanunua kwa dola milioni 40, huku Kampuni ya BAE System iliyowauzia ikimhonga dalali Saileth Vithlani, dola milioni 12 naye akawahonga wakubwa serikalini " alisema.


Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Bw. Ismail Jussa, alisema kuwa CCM imekamilisha kazi yake ya kuwaletea uhuru watanzania lakini imethibitisha kuwa haiwezi kuleta maendeleo kwa nchi hii.

"Kwa muda wa miaka 48 ya uhuru na minne ya Rais Kikwete Watanzania wameshuhudia utawala wa 'kisanii' na 'kishikaji' ambao sasa umefikia mahali pa kuvuruga umoja na mshikamano wetu kwa kushindwa kusimamia maslahi ya nchi hii," alisema Bw. Jussa.

No comments:

Post a Comment