Monday, July 13, 2009

SAKATA LA MAFUTA:Waziri Khatibu aamua kufunga mdomo

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Muhammed Seif Khatib, amesema hatazungumzia tena uamuzi wa Zanzibar kuliondoa suala la mafuta na gesi katika Muungano.
Waziri Khatib alitoa kauli hiyo jana alipoombwa kuzungumzia kama hatua hiyo iliyofikiwa wiki iliyopita si ya kuchokonoa muungano wa Tanzania.
"Suala hilo sitaki kulinzungumzia, sitazungumzia tena kwa sasa, wewe andika hivyo hivyo," alisema Khatib.


Hata baada ya kuulizwa kuwa haoni kutolitolea maelezo suala ni kuwanyima Watanzania haki ya kupata taarifa muhimu na msimamo wake akiwa waziri mwenye dhamana na Muungano, Khatib aliendelea kusisitiza kuwa hatalizungumzia suala hilo.

"Nimesema sitaki, nimeamua hivyo, ndo nishasema basi," alisema Waziri Khatib.
Wiki iliyopita, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ilitangaza kuliondoa rasmi suala la mafuta na gesi katika orodha ya mambo ya Muungano, hatua iliyoibua mjadala kutoka kwa watu wa kada mbalimbali wakiwemo wabunge na wanasiasa.


Uamuzi huo wa SMZ, ulitangazwa katika kikao cha Bajeti cha Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kinachoendelea mjini Zanzibar.
Msimamo huo ulitangazwa na Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi wa serikali hiyo Mansour Yussuf Himid.
Katika maelezo yake, waziri huyo alisema uamuzi huo ni kauli halali ya SMZ kwa kuwa umeafikiwa na Baraza la Mapinduzi katika kikao chake cha Juni 9 mwaka huu.


Mansour aliwaambia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa suala hilo, kuingizwa katika mambo ya Muungano mwaka 1968 haikuwa muafaka na kuwa Katiba ya Zanzibar Ibara ya 2 (1) inaeleza kuwa suala la usimamizi wa mafuta na gesi asilia, linapaswa kusimamiwa na SMZ.

Alifafanua kuwa uamuzi huo ulifikiwa ili kulinda alichokiita maslahi ya wananchi wa Zanzibar, jambo ambalo hata hivyo, linapingana na agizo la Rais Jakaya Kikwete la Aprili mwaka huu, katika salamu zake miaka 45 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Katika hotuba hiyo Kikwete alisema,"sioni mantiki ya kubishania kitu ambacho hivi sasa hatunacho na huenda tusikipate. Nawaomba viongozi wenzangu tusilizungumzie suala hili kana kwamba kuna uhakika wa kupatikana mafuta au yameshapatikana na kwamba kilichobakia mbele yetu ni kuzungumzia namna ya kugawana papato yake."

Wakati hayo yakiendelea Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Samuel Sitta alikaririwa na vyombo vya habari akisema Bunge la Jamhuri ya Muungano ndilo lenye mamlaka ya kuondoa vifungu vya katiba Jamhuri ya Muungano na siyo chombo kingine chochote.

No comments:

Post a Comment