Thursday, August 27, 2009

Basi laua na kujeruhi katika ajali Morogoro

Watu wanane wamefariki dunia papo hapo na wengine 52 kujeruhiwa vibaya baada ya basi la kampuni ya Scanlink walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka kijiji cha Maguha, tarafa ya Dumila wilayani Kilosa, mkoa wa Morogoro.
Ajali hiyo ilitokea Agosti 26 majira ya saa 5:15 asubuhi wakati basi hilo aina ya Scania lilipokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mwanza.
Kati ya watu waliofariki dunia wanne ni wanawake na watatu ni wanaume na mmoja ni mtoto wa kike mwenye umri wa miezi sita aliyetambuliwa kwa jina la Kwimba Sengeti, ambaye mama yake alijeruhiwa na kulazwa katika hospitali hiyo.
Marehemu wengine bado hawajatambulika na miili yao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya mkoa wa Morogoro. Majeruhi pia wamelazwa katika hospitali hiyo wakiendelea na matibabu na hali zao sio nzuri.


Watu walioshuhudia ajali hiyo walieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni utelezi baada ya mvua kunyesha katika eneo hilo na kusababisha basi hilo kuyumba na kupoteza muelekeo na kisha kupinduka.
Dereva wa basi hilo hakuweza kufahamika kutokana na hali za majeruhi waliofikishwa hospitalini kuwa mbaya.

Hata hivyo polisi kwa kushirikiana na madaktari wanaendelea kufanya uchunguzi wa kumtambua dereva wa basi hilo.
Majeruhi walionusurika katika ajali hiyo walieleza kwa masikitiko kuwa, baada ya kupata ajali hiyo walivamiwa na watu wanaoishi karibu na kijiji hicho na kuwapora baadhi ya mali zao, zikiwemo simu na fedha.
Walisema baada ya polisi kufika katika eneo hilo watu hao walitoweka na wengine kujifanya wanatoa msaada na hivyo kushindwa kubainika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba, jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi, ili kujua chanzo cha ajali hiyo.

No comments:

Post a Comment