Wednesday, August 26, 2009

Simanzi, huzuni vyatawala mazishi ya wanafunzi Iringa

Simanzi na huzuni jana zilitawala katika mazishi ya wanafunzi 12 waliofariki kwenye ajali ya moto ulioteketeza bweni lao kwenye Shule ya Sekondari Idodi mkoani Iringa.
Mamia ya wakazi wa mji wa Iringa na vitongoji vyake, viongozi wa dini, viongozi wa vyama na serikali walihudhuria mazishi hayo ya wanafunzi wa kike wa sekondari hiyo baada ya moto kuteketeza bweni lao mwishoni mwa wiki.


Kuungua kwa bweni hilo kulitokana na moto wa mshumaa uliokuwa ukitumiwa na mwanafunzi mmoja ambao ulisambaa kwenye bweni zima na kuua wanafunzi hao 12 na kujeruhi wengine 23.
Mazishi hayo yalifanyika kwa kila mwili kuzikwa katika kaburi lake huku sampuli za miili zikiwa zimechukuliwa kabla kwa ajili ya uchunguzi wa kutambua waliofariki kwenye ajali hiyo.


Salamu mbalimbali za rambirambi na michango pamoja na ahadi zilitolewa huku makampuni, serikali na hata vyama vya kisiasa vikiahidi kusaidia ujenzi wa majengo yaliyoteketea pamoja na kusaidia vifaa kwa wanafunzi walionusurika maisha.
Serikali iliagiza wakaguzi wa elimu wa kanda na wilaya nchini kufanya ukaguzi kwenye mabweni yote ya shule za binafsi na serikali kuangalia kama yana milango ya kutosha ya kuweza kutumika nyakati za dharura.


Akizungumza jana kwenye mazishi hayo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe alisema kuwa wakaguzi hao wanapaswa kuhakikisha nyenzo zote za usalama zinakuwapo, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kuzimia moto na vile vya kutambua moto na moshi.
Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Ruaha, Dk Donald Mtetemela alisema kuwa, imefika wakati serikali na wajenzi wakasema basi juu ya majanga ya moto kwa wanafunzi kwa kuchukua tahadhari mapema kuhakikisha mabweni yana vifaa vyote iwapo kunatokea ajali za moto.


Naye mkuu wa mkoa, Mohammed Abdulaziz alisema kuwa, zimechukuliwa sampuli za miili yote 12 ili kuweza kupima vinasaba vitakavyowezesha kutambua miili ya waliofariki na kuwawezesha wazazi na ndugu kujua makaburi ya waliofariki.
Makaburi hayo pia yamewekwa alama.
Pia alisema serikali itafanya uchunguzi wa kina kuweza kubaini chanzo cha moto huo na jinsi ulivyosambaa katika vyumba vyote.


CCM mkoani Iringa na makao makuu wametoa mablanketi 66 kwa ajili ya wanafunzi walionusurika, huku kampuni ya huduma za simu za mkononi ya Vodacom ikiahidi kusaidia ujenzi.
Akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo, wakiwemo walionusurika katika ajali hiyo na wazazi wao, Waziri Maghembe alisema ajali hiyo ni kubwa na inatia huzuni kwa wanafunzi, wazazi na majirani wanaoishi katika eneo hilo na endapo shule haitafungwa, itakuwa ni hatari kubwa kwa wanafunzi walionusurika.


Alisema wanafunzi 326 walionusurika hawana mahali pa kulala baada ya bweni hilo kuteketea, ambalo lilikuwa na vyumba 25 na uwezo wa kuchukua watu 461, kuteketea kabisa kwa moto huo uliozuka usiku wa manane Agosti 23 mwaka huu kutokana na mshumaa uliokuwa ukitumiwa na mwanafunzi mwenzao, Naomi Nyange.

Maghembe alisema, kuwa shule hiyo imefungwa rasmi Agosti 23 na itafunguliwa Septemba 13 mwaka huu ili kutoa nafasi kwa serikali kufanya ukarabati wa bweni hilo.

No comments:

Post a Comment