Tuesday, August 25, 2009

fidia waathirika wa mabomu Mbagala ni aibu tupu.

Fidia kwa waathirika wa milipuko ya mabomu iliyotokea Aprili 29 mwaka huu katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) Mbagala Kizuiani jijini Dar es Salaam, ilianza jana huku wengi wakilalamika kuwa kiasi walichopata ni kidogo.
Hadi jana alasiri, mtu aliyekuwa amelipwa fidia kubwa alipata kiasi cha Sh11 milioni, wakati aliyelipwa kiasi kidogo zaidi alipata Sh30,000 (takriban mifuko miwili ya saruji), malipo yaliyosababisha malalamiko mengi.


"Nyumba yangu nilijenga kwa Sh28 milioni ikiwa na vyumba sita, lakini leo nimelipwa Sh1.6 milioni tu huu ni udhalilishaji," alisema Obedi Samamba wa Mtaa wa Mbagala Kuu.
Alisema fedha hizo hazitoshi hata kujenga chumba kimoja kwani, gharama za vifaa vya ujenzi, ikiwemo mifuko ya sarujii na mabati, imeongezeka kwa kiasi kikubwa.


Alifafanua kuwa kama alijenga nyumba wakati huo kwa gharama za Sh28 milioni, anastahili fedha zaidi, ili aweze kujenga nyumba nyingine.
Ramadhan Shaaban, ambaye alipata hundi ya Sh4 milioni, alisema kiasi hicho cha fedha hakitoshi kujenga nyumba zake mbili zilizokuwa zimebomoka kabisa eneo la Mbagala Kuu.


"Kwa ujenzi wa nyumba zangu zote mbili kiasi hiki hakitoshi chochote Sh1 milioni ni malipo ya fundi tu; vifaa vya ujenzi na mahitaji ya vitu vingine vitagharimu shilingi ngapi," alihoji.
Shaaban, aliyezungumza kwa manung'uniko makubwa, alieleza kuwa ni mapema mno kwake kujua cha kufanya, baada ya kupata hundi hiyo, lakini kimsingi, malipo hayo yanamkatisha tamaa.
"Siwezi kusema nini niamue kwa sasa kwa kuwa serikali imeshatoa uamuzi wake, lakini kiwango hiki kinakatisha tamaa," alisema Shaaban.
Mkazi mwingine, Kaizi Salum alipigwa na butwaa baada ya kupata hundi ya Sh30,000.

"Nilikuwa sijamalizia kujenga nyumba yangu, lakini tangu nimeanza ujenzi nimetumia Sh3 milioni. Nashangaa kupata fidia ya Sh 30,000 tu," alisema.
Wakati waathirika hao wakilalamikia malipo kidogo, Araf Hamed mwenye nyumba namba MA/1/303, alijikuta akikosa hundi yake licha ya kusaini kitabu cha utambuzi.
Hamed aliiambia Mwananchi akisema: "Nilipotaka kusaini kitabu cha pili cha kukabidhiwa hundi, niliambiwa hundi yangu haijafika na kwamba niendelee kufuatilia."


Zaidi ya wakazi 300 wa Mtaa wa Mbagala Kuu walijitokeza kwenye ofisi za halmashauri ya Manispaa ya Temeke jana kuchukua malipo ya fidia zao.
Mkuu wa wilaya ya Temeke, Said Mkumbo aliwaambia waandishi wa habari kuwa fidia hiyo itatolewa na kumalizika katika kipindi cha mwezi mmoja na utaratibu ni kwamba kila mtaa na siku yake.
Alisema wameanzia na Mtaa wa Mbagala Kuu, ambako zaidi ya watu 2,307 walioathirika na milipuko hiyo, walijitokeza kudai fidia zao na madai yao kukubaliwa.


"Huu ndio mtaa wenye watu wengi zaidi walioathirika kuliko mtaa mwingine wowote. Baada ya kumaliza kuwalipa, tutahamia mtaa mwingine,"alisema Mkumbo.

Hata hivyo, utaratibu huo ulionekana kutoeleweka kwa waathirika wengi kutokana na wakazi wa maeneo mengine kufika pia kwenye ofisi hizo wakitarajia kulipwa fidia zao.
Wengi walitaka serikali kutoa taarifa mapema ya utaratibu wa kulipa fidia badala ya hali ilivyo sasa inayofanya wengi kupoteza muda bila lazima.


Serikali imetenga Sh8.5 bilioni kwa ajili ya kulipa fidia kwa watu walioathirika kwenye milipuko hiyo iliyoua zaidi ya watu 26, kujeruhi na kuathiri takriban nyumba 9,000, ambazo zilibomolewa ama kuharibiwa.

No comments:

Post a Comment