Monday, August 3, 2009

Hamad Rashid: Kikwete jiuzulu.

Kiongozi wa Upinzani bungeni Hamad Rashid Mohamed, amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kujiuzulu kutokana na kile alichosema ni serikali yake kushindwa kufanya kazi hivyo kukosa imani kwa wabunge wa chama chake Chama Mapinduzi (CCM).

Shinikizo hilo la upinzani linakuja wakati hali ya kisiasa nchini ikiwa tete huku Bunge na serikali ya Rais Kikwete, zikiwa katika msuguano wa utekelezaji wa baadhi ya mambo mazito ikiwemo hatua za kuchukua kwa watumishi waandamizi wa umma waliotajwa katika sakata la mkataba wa kifisadi wa Richmond.

Ikulu kupitia Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo tayari imemkingia kifua Rais katika sakata la Richmond ikisema alichukua hatua madhubuti ikiwemo kuzuia malipo, Hamad akizungumza mjini Wete juzi, alisema kwa jinsi mjadala wa Richmond ulivyokwenda na wabunge hasa wa CCM kuikosoa serikali yake, mkuu huyo wa nchi hana budi kuachia ngazi kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea kwani serikali yake imeshindwa kazi.

"Kikwete amepandikiza mpasuko Zanzibar badala ya kuushughulikia, itamtapikia nyongo" alitahadharisha na kusema kwa lolote litakalotokea atabeba lawama kwani ameshindwa kuchukua hatua mbalimbali zinazostahili katika matatizo yanayotokea nchini.

Hamad akitoa mfano, alisema nchini Uingereza pindi kiongozi wa serikali akipata matatizo kama yanayotokea nchini na watu wa chama chake wakakosa imani na serikali huamua kujiondoa ili kuwekwe serikali mpya na kuongeza: "Na hili ndilo anatakiwa kufanya Kikwete."

Kauli hiyo ya kiongozi wa upinzani inakuja pia katika kipindi ambacho wabunge wa CCM ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kuisulubu serikali ya Rais Kikwete, katika mambo mbalimbali ya ufisadi huku wakionyesha dhahiri kutoridhishwa na hatua za kupambana na tatizo hilo.

Ingawa Hamad hakutaja majina ya wabunge, lakini Mbunge wa Kyela Dk Harrison Mwakyembe, Christopher Ole Sendeka (Simanjiro), Anne Kilango Malecela (Same Mashariki), Fredi Mpendazoe, John Shibuda (Maswa), Herbet Mtangi (Muheza), ambao wote ni kutoka CCM juzi wakiongozwa na Spika Samuel Sitta, wamekuwa wakiibana serikali bungeni kuhusu mambo mbalimbali ya ufisadi na kutaka hatua zichukuliwe kwa watuhumiwa.

Juzi wakati wa mjadala wa Richmond, baadhi ya wabunge waliibana serikali katika sakata hilo na kuhoji iweje serikali ishindwe kuwachukulia hatua watu kama Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Dk Edward Hoseah, Mwanasheria Mkuu (AG) Johnson Mwanyika, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Athur Mwakapugi, Kamishna wa Nishati Bashir Mrindoko na wajumbe wote wa Timu ya Ushauri katika Mikataba ya Serikali (GNT) kutoka Benki Kuu (BoT) Ofisi ya AG na Shirika la Umeme (Tanesco).

Wadadisi wa mambo ya kisiasa wanachukulia moto uliowashwa juzi na wabunge wa CCM katika sakata la Richmond na azimio la Bunge kuipa serikali muda hadi Novemba, iwe imeshughulikia watumishi wote waandamizi, ni ishara mbaya kwa serikali ya CCM na Rais Kikwete.
Udadisi huo wa hali tete ya kisiasa na udugu wa mashaka kati ya wabunge na serikali, unadhihirishwa na kauli ya Ikulu ambayo ilitolewa na Luhanjo ghafla jioni, baada ya Bunge kuazimia huku wabunge wa CCM wakiwa vinara waliowasha moto huo wakiongozwa na Spika kwa ushirikiano na baadhi ya wabunge wa kambi ya upinzani.


Ikulu ilitaja mambo manne ya msingi ambayo Rais alishiriki katika Richmond, ikiwa ni pamoja na kuzuia malipo kwa kampuni hiyo baada ya kutiliwa mashaka. Hamadi akizungumzia zaidi hali hiyo kati ya wabunge wa CCM na imani yao kwa Rais, alisema kwa uadilifu kiongozi huyo alipaswa kujiuzulu ili uchaguzi ufanyike.

Kuhusu uchaguzi Tanzania kutarajia vitambulisho vya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), alisema hilo ni kosa kubwa na ukiukwaji wa sheria.
Hamad alikuwa akieleza wananchi hao kwamba, chaguzi zote zinazofanyika kwa kutumia daftari la Zanzibar ni batili na kuongeza kwamba, Rais Kikwete anajua hilo, lakini amekuwa akilifumbia macho kwa maslahi ya chama chake.


"Tunachohitaji ni daftari tofauti kwa Zanzibar na Muungano ili watu wapige kura kwa haki kinyume cha hapo watamuunganisha Kikwete na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ambaye anaandaliwa mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya The Hague."

Tangu Rais Kikwete kuingia madarakani mwaka 2006, serikali yake imekuwa ikikabiliwa na misukosuko ambao mmoja mkubwa unaoitikisa hadi sasa ni mkataba wa kifisadi wa Richmond, uliotiwa saini Juni 23 mwaka huo.

Richmond ambayo ilimfanya Edward Lowassa kujiuzulu Uwaziri Mkuu imekuwa ikiitikisa serikali tangu Mkutano wa 10 wa Bunge la mwezi Aprili, mwaka jana.
Bunge lilitoa maazimio 23 kutaka serikali itekeleze ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kwa maafisa hao waandamizi wa serikali, lakini wiki iliyopita serikali ilitoa taarifa bungeni ambayo iliwasafisha.


Hali hiyo iliibua upya moto wa Richmond huku wabunge wa CCM wakiongozwa na Spika wakiwa mwiba kwa serikali ya Rais Kikwete, huku mbunge wa Maswa Shibuda akitaka iwepo sheria itakayolipa Bunge meno zaidi ya kuing'ata serikali hasa inaposhindwa kuwajibika kwa Bunge.

No comments:

Post a Comment