Monday, August 3, 2009

Moto wateketeza bweni Chuo cha Polisi.

Wiki moja baada ya kutokea majanga makubwa ya moto na kuteketeza ghala la kuhifadhia makreti ya bia na mwingine kuteketeza meli, jana tena moto umeteketeza bweni zima katika Chuo Kikuu cha Polisi na kusababisha hasara kubwa ambayo haijafahamika.

Moto huo ambao chanzo chake hakijajulikana ulianza majira ya saa tisa alasiri na kuteketeza bweni la Solomon Lian lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 90 kwa mara moja.
Hali ya taharuki iliibuka chuoni hapo baada ya tukio hilo la ghafla kutokea na hasa ikizingatiwa liko karibu na makazi ya watu.


Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Chuo Elise Mapunda alisema kuwa moto huo uliolipuka ghafla uliliteketeza bweni zima la Solomon Lian.

"Moto ulianza saa tisa na dakika kumi alasiri na kuteketeza bweni hilo lenye vyumba 30 na kila chumba wanakaa wanafunzi watatu na kila chumba kuna kitanda godoro, meza, viti na vitanda vyote vimeteketea,"alisema mkuu huyo wa chuo.

Alisema mpaka sasa chanzo cha moto huo hakijagundulika na hakuna mtu aliyeathirika, bweni lilikuwa halina wanafunzi sababu walishaondoka kwenda likizo.
Hata hivyo alisema kwa wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hii alikuwa na kikao ingawa hakusema kikao hicho kinahusu nini.


Kuhusu hasara iliyopatikana kutokana na moto huo alisema kikao cha Ujenzi na Boharia Mkuu wa Jeshi la Polisi ndiyo atakayeelezea hasara iliyopatikana kutokana na moto huo.

"Moto huu umetushtua sana, umeibuka katika wakati ambao hatukutarajia na hakuna kitu tulichookoa kutoka katika bweni hilo la wanafunzi,"alisema mkuu huyo.
Wiki iliyopita meli ya mizigo ya Mv Pemba inayomilikiwa na Kampuni ya Azam Marine, iliteketezwa kwa moto katika Bandari ya Dar es Salaam.


Meli hiyo ilishika moto saa 4:20 asubuhi, ikiwa imeegeshwa kandokando ya Bandari ya Dar es Salaam eneo la boti ziendazo kwa kasi jijini Dar es Salaam. Inadaiwa kuwa chanzo cha moto huo ni mafundi waliokuwa wakichomelea ndani ya meli hiyo iliyokuwa ikikarababitwa.

Licha ya vikosi vya zimamoto vya Mamlaka ya Bandari na Halmashauri ya Jiji Dar es Salaam kufanikiwa kuuzima moto huo, sehemu yote ya ndani ya meli hiyo iliteketea.

No comments:

Post a Comment