Saturday, August 1, 2009

Wanafunzi Chuo kikuu Tumaini wakerwa na Askofu.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini wameipinga kauli ya Mkuu wa Chuo hicho, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania (KKKT), Alex Malasuasa ya kuongeza ada ya mwaka wa masomo 2009/10 kwa asilimia 60.

Bwana Malasusa alinukuliwa hivi karibuni akisema kwamba nyongeza hiyo, haiwezi kuondolewa kwa kuwa lengo ni kukabiliana na ongezeko la gharama za uendeshaji.
Chuo hicho, kilipandisha ada ya mwaka kutoka Sh1.5 milioni hadi kufikia Sh2.6, kiwango ambacho wanafunzi wengi wanasisitiza kuwa kitasababisha wengi washindwe kuendelea na masomo.


Wanafunzi hao wamesema kauli ya Malasusa inaonyesha ubabe na kamwe haiwatendei haki wanafunzi kwa sababu wengi wao wanatoka katika familia zenye kipato cha chini.
Hata hivyo, walisema hawajakata tamaa na bado wataendelea kuubana uongozi ili kiwango hicho kipunguzwe.


"Mzazi wangu kwa kweli hawezi kulipa kiwango hicho cha ada. Ninachoomba ada hiyo ibakie ile ile ya mwanzo," alisema mwanafunzi wa mwaka wa pili, Esnath Mayemba.

Denis Mwasawanga alisisitiza kuwa huduma zinazotolewa na chuo bado ni duni na haoni sababu yoyote ya kuwepo kwa nyongeza hiyo.

"Kwanza hiyo ada iliyokuwepo ilikuwa kubwa kuliko hata huduma tunazopata. Chuo tunasoma tu theory (nadharia) hakuna practical (kwa vitendo), hakuna studio," alilalamika Mwasawanga, mwanafunzi wa mwaka wa pili.
Hata hivyo, Waziri wa Habari wa serikali ya wanafunzi, Joseah John alisema viongozi wenzake wamekuwa wakijaribu kuwasiliana na uongozi wa chuo na kwamba wamebaini kwamba kuna nafasi ya kutatua suala hilo kwa mazungumzo.
"Siku zichache zijazo nitakuwa tayari kueleza mchakato mzima wa mauzungumzo hayo," alisema Joseah.

No comments:

Post a Comment