Tuesday, August 4, 2009

mgomo TRL.

Wafanyakazi wa Kampuni ya Reli nchini (TRL), jana walianza kwa mbinu mpya mgomo wao wa muda usiojulikana, ili kuushinikiza uongozi wa kampuni hiyo kusaini mkataba wa hiari unaohusu mkono wa heri.
Mgomo huo ulianza mchana kwa sala na dua baada ya kumalizika mkutano wao na viongozi wa Chama Cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu) uliofanyika katika Ukumbi wa Karakana ya Makao Makuu ya TRL, jijini Dar es Salaam.
Hatua ya mgomo ilifikiwa baada ya viongozi wa Trawu kuwaambia wafanyakazi hao kuwa TRL wamegoma kusaini mkataba huo unaojumuisha mafao ya wafanyakazi.
Habari za uhakika zimeeleza kuwa Bodi ya TRL iliyoketi hivi karibuni nchini INDIA, imegoma kusaini kipengele cha 'mkono wa heri' kilichomo kwenye mkataba wa hiari wa kampuni hiyo.
Katibu Mkuu wa Trawu, Sylvester Rwegasira aliwaambia wafanyakazi hao jana kuwa Julai 29, mwaka huu walikubaliana kukutana na Bodi ya TRL kwa ajili ya kupewa taarifa za kikao kilichofanyika INDIA lakini uongozi huo wa kampuni hiyo, haukutokea katika kikao hicho.
"Awali wafanyakazi wa TRL walitaka kugoma ili uongozi ukubali kusaini mkataba wa hiari, lakini tuliwazuia na uongozi uliahidi kuwa utakaa na kujadili mkataba huo na kikao hicho kilifanyika INDIA," alisema Rwegasira na kuongeza:
"Baada ya kikao hicho kufanyika na viongozi kurudi nchini, Trawu tulitaka kujua maafikiano yaliyofikiwa kwa kuomba kukutana na Bodi ya Wakurugenzi Julai 29, mwaka huu, lakini siku ya kikao, Mkurugenzi wa TRL hakutokea na akatuma barua kuwa kikao kitafanyika siku nyingine".
Rwegasira ambaye alizungumza na wafanyakazi hao wapatao 500 kwa jazba, alisema kitendo cha mkurugenzi huyo kutotokea katika kikao hicho, kimeonyesha jinsi anavyowadharau.
"Hili ni tatizo ambalo hatuwezi kulivumilia kwa sababu mkataba uliopo ni ule tuliosaini na kampuni hii ikijulikana kama Shirika la Reli Tanzania (TRC). Kwa ujumla baada ya kuja mwekezaji ilitakiwa tusaini mkataba mwingine kati ya Trawu na TRL na hili ni lazima lifanyike, lakini inaonekana viongozi wa TRL wanagoma; kwa hiyo kinachofuata hapa wafanyakazi nafikiri mnakijua," alieleza Rwegasira.
Rwegasira ambaye hakutaja waziwazi kwamba anawataka wafanyakazi hao wafanye mgomo, alisema; "Jamani anayetaka kufika peponi lazima afe na hata ukiambiwa na mkubwa wako ingia msituni unaingia, akikwambia toka unatoka. Kama wao wamesema watapanga siku tuzungumze nao tutasubiri mpaka lini, kazi kwenu," alisema kwa jazba.
Rwegasira aliitupia lawama serikali kuwa wamekuwa wakipeleka malalamiko kuhusu mwenendo mzima wa TRL, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kuinusuru kampuni hiyo ambayo kadri siku zinavyozidi kwenda utendaji wake umekuwa wa kubahatisha.
Baadaye Rwegasira alidai kuwa hakuzungumza na wafanyakazi hao kama sehemu yao bali alikuwa akiwapa taarifa akiwa kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli ili wenyewe wapime cha kufanya.
Baadhi ya wafanyakazi hao walidai kuwa baada ya kikao hicho, wameamua kugoma kufanya kazi hadi hapo uongozi wa TRL utakapokubali kusaini mkataba huo.
Kabla ya kuanza kikao hicho wafanyakazi wa kampuni hiyo waliomba dua ili uongozi wa TRL ukubali kusaini mkataba huo.
"Kutokana na dharau hizi na kutotaka kututekelezea madai yetu, hakuna jingine zaidi ya kugoma mpaka hapo watakapokaa na kujadili mkataba. Hatuwezi kuendelea na kazi," alisisitiza Mohammed Chamwimba mmoja wa wafanyakazi hao huku akishangiliwa na wafanyakazi wenzake. Aliendelea:
"Sisi tupo tayari kulipwa haki zetu zote halafu na ni sisi tutakaoamua kuendelea na kazi au laa na ili tulipwe inatakiwa tugome la sivyo tutapelekwa kama gari bovu.” Msemaji wa TRL Midladjy Maez alipotakiwa kuzungumzia suala hilo jana alisema hajui lolote na kuwataka waandishi wakaandike lolote wanalolijua.
"Mimi sijui lolote kama kuna mgomo, kwanza nyie mkisikia kuna tatizo ndio mnakuja hapa, mbona mazuri ya TRL huwa hamwandiki, kaandikeni lolote mnalolijua," alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa TRL hakupatikana ofisini kwake kuzungumzia suala hilo na hata simu yake ya mkononi ilikuwa imezimwa.

1 comment:

  1. hey, fresh blog check out mine as well> Dem YoungEntertainment> http://aka-alter.blogspot.com/

    ReplyDelete