Monday, August 24, 2009

Hatima ya wafanyakazi TRL leo

Macho na masikio ya Watanzania leo yanaelekezwa katika kikao kitakachoamua hatima ya Uongozi wa Kampuni ya Reli nchini (TRL), kuendelea kukaa ofisini au kuondoka.
Hatima ya wawekezaji hao kutoka India itafahamika baada ya kumalizika kwa kikao kitakachotoa maamuzi ya kusaini mkataba wa hali bora kazini na mkono wa heri kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo ama kutosainiwa kwa mkataba huo.


Kikao hicho kitawakutanisha Chama Cha Wafanyakazi wa Reli nchini (TRAWU) na uongozi wa TRL katika Ofisi za Makao Makuu ya kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka ndani ya TRAWU na uongozi wa TRL vinasema, wafanyakazi hao wamefikia hatua hiyo kutokana na walichodai kuwa ni kuchoshwa na usumbufu wa uongozi wa TRL.

"Mkataba wa makubaliano (MOU) ulisainiwa hivi karibuni, lakini ilipofika wakati wa kusaini mkataba wenyewe wakazua hoja mpya kwa lengo la kutaka mkataba huo usisainiwe," kilisema chanzo kimoja cha habari na kuongeza:
Katika hatua nyingine vyanzo hivyo vilidai kuwa mbali na uamuzi wa kuwafungia wawekezaji hao milango ili wasiingie tena ofisini, pia wana lengo la kuionyesha serikali kuwa wana uwezo wa kuwaondoa hao wahindi ingawa serikali inawatetea.


"Sisi tuna uwezo wa kuwaondoa na maamuzi ya Jumatatu hayawezi kubadilishwa hata kwa dawa, isipokuwa njia pekee ni kuwataka waondoke" kiliongeza chanzo kingine.
Wakati wafanyakazi hao wakifikia hatua hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa TRL Hundi Chaudhary alisema yeye hakatai kusaini mkataba huo bali bado wanaendelea na mazungumzo.

"Sio kuwa sitaki kusaini mkabata huo isipokuwa bado tunaendelea na mazungumzo na Jumatatu tutakuwa na kikao kingine hapa ofisini kwangu"alisema Chaudhary na kuongeza:
"Pengine kikao hicho cha Jumatatu ndiyo kitakachotoa mwafaka ama tunaweza kuwa na kikao kingine baada ya hicho".

No comments:

Post a Comment