Monday, August 10, 2009

Wahadhiri vyuo vikuu nchini kugoma.

Wahadhiri wa vyuo vikuu sita vya umma wameamua kutimiza azma yao ya muda mrefu ya kugoma kufundisha, kuishinikiza serikali kutimiza ahadi yake ya kuwalipa malimbikizo ya posho za pango pamoja na kuboresha viwango vya mafao ya kustaafu.

Mwezi Juni mwaka huu,mwenyekiti wa Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (Udasa), Dk Damas Nyaoro alikaririwa akisema kuwa tangu waiandikie serikali mwezi Aprili kuhusu madai yao, bado hawajajibiwa na kwamba kutokana na kimya hicho wana mpango wa kuitisha mgomo.

Jana viongozi wa wahadhiri kutoka vyuo hivyo vya umma walikutana na kufikia maazimio ya kugoma hadi watakapotimiziwa madai yao kama kikao cha Wizara ya Fedha kilichopangwa kufanyika Agosti hakitatoa jibu la kuridhisha.

Waraka huo wenye namba SUASA/S.1/ wa Agosti nane mwaka huu umetaja maazimio sita ya wahadhiri hao.
Wahadhiri hao walisema kuna haja ya serikali kuchukua hatua za haraka kuliainisha suala la wahadhiri wastaafu wanaokabiliana na hali ngumu baada ya kustaafu kutokana na mafao finyu ya PPF (Mfuko wa Pensheni ya Mashirika ya Umma) na SSS (Senior Staff Superannuation Scheme).


"Jopo la mawakili mahiri limeshakabidhiwa kazi ya kuwafungulia mashtaka PPF kwa kulipa mafao mabovu kwa wastaafu wa vyuo vikuu," inaeleza sehemu ya waraka huo wa wahadhiri.

Wahadhiri hao waliazimia pia kwamba menejimenti za vyuo vikuu ziwaruhusu waajiriwa wapya kujiunga na mifuko ya pensheni wanayoitaka.
Wahadhiri hao walisema wamechoshwa na ahadi zisizotimizwa hivyo itabidi wafanye vitendo kwani muda mwingi wamekuwa wakipewa ahadi nyingi kuhusu madai yao, lakini hakuna inayotekelezwa hivyo kugoma kufundisha na kufanya kazi kutaifanya serikali kuchukua hatua za makusudi.


Walisema kuwa zipo nyaraka za ushahidi za mjadala uliofanywa na serikali Oktoba 19, 2004 kuhusu mafao madogo kwa wastaafu wa vyuo vikuu, lakini hakuna maendeleo yoyote yaliyokwishafanywa kwa wastaafu hao.

Walisema kwa muda mrefu suala hilo lipo serikalini, lakini hakuna huruma yoyote kutokana na masharti wanayopewa na mpango huo wa wafanyakazi waandamizi wa SSSS kwa walimu wanaoendelea kustaafu katika vyuo hivyo.

"Aprili 2009 PPF waliahidi kutoa taarifa Mei/Juni kama wameamua kuongeza mafao kwa wastaafu hao, badala yake wamejibu Agosti 6, lakini majibu hayajaturidhisha chochote zaidi ya kuona hawako makini na kile wanachokifanya," inaeleza taarifa ya wahadhiri hao.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa Sheria ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2008 inaruhusu mfanyakazi yeyote mpya kuchagua mfuko wa mafao anaoutaka, hivyo uongozi wa vyuo vyote vya umma nchini unapaswa kuwapa nafasi wafanyakazi hao kuchagua mifuko mizuri ya kujiunga.

"Utawala wa vyuo hivi unapaswa kuwaruhusu wafanyakazi wake wapya kuchagua mfuko wa mafao yao ambao utakuwa na faida na si kuwalazimisha kujiunga na PPF kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa viongozi wengi vyuoni,"alisema Dk Nyaoro.

Aliongeza uvumilivu wao katika kusubiri kutatuliwa matatizo yao, unaonekana hauna maana yoyote, hivyo inabidi wafanye vitendo.

"Kama mtu unaamua kuwa mvumilivu na mstaarabu kwa kuamini utatimiziwa ulichoahidiwa na kisitekelezwe, hakuna haja ya kuendelea kuumia wakati zipo njia nyingi za kukutoa katika maumivu hayo," alisema Dk Nyaoro.
Alisema wana uhakika mfuko wa PPF una uwezo wa kulipa mafao mazuri kwa wastaafu tofauti na ilivyo sasa, lakini cha kushangaza ni vile ambavyo wahusika wamekuwa wakilichukulia kirahisi suala hilo na hawajui jeuri na kiburi hicho wanakipata wapi.


Akizungumza katika kikao hicho, mwenyekiti wa wahadhiri wa Chuo Kikuu Cha Tiba na Sayansi cha Afya Muhimbili (Muhas), Dk Thomas Nyambo alisema inabidi wasikilizwe madai yao kwani itafikia wakati malipo ya posho za pango yanayolimbikizwa yatakuwa makubwa kiasi cha serikali kuhisi inahujumiwa na vyuo hivyo.

"Fedha hizo ni kiasi kidogo sana kwa mwezi ukilinganisha na hali ya maisha ya sasa, lakini zinapolimbikizwa na kuwa nyingi itafikia mahali serikali itaona kama vyuo vinataka kuwafilisi,"alisema Nyambo.
Dk Nyambo alisema awali serikali iliahidi kulipa posho ya pango kwa kila mwezi, ila imekuwa ni kinyume na badala yake fedha hizo zinalimbikizwa kiasi cha kuwa kikubwa, jambo linaloweza kusababisha matatizo wakati wa kuzilipa.


Akitoa mfano wa watu waliopokea mafao madogo kutoka mfuko huo licha ya kufanya kazi kwa muda mrefu na kwa umakini, makamu mwenyekiti wa Udasa, Mushtaq Osman alisema ni jambo la kushangaza na kusikitisha kwa mstaafu kama Marehemu Profesa Othman Harub kupokea kiasi cha Sh21 milioni tu kama mafao.

"Upo umuhimu mkubwa wa serikali kushinikiza PPF/SSSS kutoa fedha za kutosha kwa wastaafu... cha kushangaza ni jinsi ambavyo PPF wamekuwa hawajali suala hili na kuona kama ni wimbo tu tunawaimbia,"alisema Profesa Osman.

Viongozi waliohudhuria mkutano huo ni kutoka UDSM, Muhas, Chuo Kikuu cha Elimu (Duce), Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Mzumbe (Mucasa) kilichoko Morogoro na Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Stadi za Biashara (Mucobs).

No comments:

Post a Comment