Friday, September 25, 2009

Korea yatangaza kununua ardhi kubwa Tanzania, serikali yakana

Serikali imesema kuwa taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari vya Ulaya kuwa imeuza ardhi ya ukubwa wa kilomita za mraba 1000 za kilimo kwa Korea ya Kusini kwa ajili ya matumizi ya kilimo si za kweli.

Taarifa zilizotolewa jana na vyombo hivyo zilieza kuwa Korea Kusini imekubaliana na serikali ya Tanzania kufikia hatua hiyo ikiwa ni sehemu ya makubaliano kati ya mataifa masikini na tajiri duniani.
Afisa wa Shirika linaloendeshwa na Serikali ya Korea linaloshughulikia maendeleo ya kilimo vijijini, Lee Ki-Churl, alinukuliwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), akisema kwamba mkataba huo utasainiwa mwezi ujao.


Kwa mujibu wa taarifa hizo, mkataba wa makubaliano kati ya mataifa hayo mawili ni matokeo ya ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyoifanya katika mataifa ya mashariki ya mbali.
Akizungumza jana, Waziri wa Kilimo na Chakula na Ushirika, Steven Wasira, aliliambia gazeti dada la hili la The Citizen kuwa hakuwa na taarifa na mkataba huo.


"Nilikuwa sehemu ya ujumbe wa Waziri Mkuu Korea Kusini na kilichotokea kule hakikuwa zaidi ya kuwakaribisha wawekezaji wa kigeni katika sekta zote ikiwamo ya kilimo."

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Emmanuel ole Naiko alikanusha na akasema hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa na serikali katika kilimo na Korea Kusini.

No comments:

Post a Comment