Tuesday, September 15, 2009

Polisi Pemba Wakanusha Kukipendelea Chama cha CUF

Jeshi la Polisi kisiwani Pemba limekanusha taarifa zilizochapishwa na baadhi ya vyombo vya habari zinazodai kuwa linafanya kazi zake kwa kukipendelea chama cha CUF.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti makamanda wa polisi wa mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba wamesema taarifa hizo si za kweli na zimelenga kuchafua jina zuri la jeshi la polisi kisiwani Pemba ambalo kwa sasa linafanya kazi zake kwa mashirikiano makubwa na jamii huku jamii wakiliunga mkono na kuona polisi ndio mahala pa kukimbilia.

Akitoa ufafanuzi kamanda wa polisi wa mkoa wa Kusini Pemba Said Salum Malekano amesema Shutma zilizotolewa na Katibu wa CCM wa Wilaya ya Chake Chake Zainab Shomar na kukaririwa na Vyombo mbali mbali vya habari kwamba Jeshi la polisi lilishindwa kuwatawanya Vijana wa CUF waliokuwa wakidai kupatiwa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi halina msingi kwani kiklichojitokeza ni jeshi la Polisi kutumia njia ya kidiplomasia kukabiliana na hali iliyokuwepo badala ya kutumia nguvu.

Amesema hata hivyo wakati Jeshi la polisi likiwa limeshafikia makubaliano na Viongozi wa CUF juu ya kuwatawanya Vijana wao ndipo kwa mshangao waliposhuhudia ujio wa askari wa jeshi la Wananchi.

“Kama tunaonekana sisi ni washabiki wa CUF kwa kuwa hatukutumia nguvu, huo ni mtazamo wake lakini sisi kama Jeshi la polisi hatutatumia nguvu mahala ambapo hapastahiki na badala yake tutatumia misingi ya kisheria katika kutekeleza majukumu yetu” alisema Malekano.

Kwa upande wake akijibu shutuma za kushindwa kuwazuia wafuasi wa CUF wasiingie katika eneo la vituo vya kuandikishia, kamanda wa polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Yahya Rashid Bugi amesema kazi ya jeshi la Polisi ni kusimamia amani na utulivu na kulinda usalama wa raia na mali zao.
Hivyo kwakuwa hapakuwepo na kitendo kilichohatarisha amani moja kwa moja au uharibifu wa mali jeshi hilo halikuona sababu ya kutumia nguvu ya ziada kupambana na wananchi hao ambao hawakuwa wa chama cha CUF pekee.

Bugi amewataka wanasiasa kufanya kazi zao za kisiasa na kuviacha vyombo vya dola kufanya kazi zake zake ambazo ni za kitaalamu zaidi na zinahitaji kuendeshwa kwa kuzingatia misingi ya kisheria.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa kisiwani Pemba wamezipokea shutuma hizo kwa mtazamo tofauti.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Aliens For Femars party (AFP) Sudi Said Sudi amesema jeshi la polisi kisiwani Pemba lilifanikiwa kukwepa mtego wa cuf wakuleta vijana kwa wingi kwa madai ya kujiandikisha ili polisi wawavamie na kuwapiga ilijeshi hilo lipate kulaumiwa.

Alisema njia ilizozitumia za kutumia busara ni njema sio tu kwao lakini kwa upande wa dimokrasia nchini Tanzania na hivyo kudhihirisha maboresho ya jeshi la polisi tunayoyasikia yakitangazwa kila siku kwenye vombo vya habari na viongozi wa jeshi hilo.

Alisema inavyoonekana katibu huyo wa ccm wilaya chake bi Zainabu Shomar aliye kalia kiti hicho kwa muda wa miezi miwili iliyopita ni mchanga kwa siasa za Pemba kuna haja ya viongozi wake waliobobea kumueka chini kumfundisha namna ilivyo badala ya kumuacha kuchezea vyombo ambavyo havihusiki na siasa.

Aidha mwenyekiti wa UDP Mkoa kusini Pemba Asha Mohamed Ali amesema hizo ni sera za chama cha CCM kutumia vyombo vya habari kuzungumza mambo ambayo hayapo kwa lengo la kutaka kuanzisha fujo kwavile wanaelewa kuwa wao wana vyombo vya dola.

Alisema haingii akilini wala hakuna atakaemkubali kuwa polisi Pemba ni wa CUF ila anachoona yeye labda hakubaliani tu na uwelewa na utaratibu walionao polisi hivi sasa wa kushirikiana na jamii katika program zake.

Nae mwenyekiti wa TLP Ziada Khalfani Said alisema kauli ya katibu huyo siya kushangaza kwa vile siasa za mwaka huu ni ngumu zinahitaji kutafuta mbeleko zaidi hivyo hio ni njia tu ya kutaka vyombo vya dola kama vile majeshi yeye alioyasifu anadhani yataweza kuwasaidia.

“kama mtazamo wa CCM pemba kufanya kazi kwa polisi ni kama vile zamani kupiga na tukawapa majina melodi leo wanapiga wapi ilivyo kuwa zamani kutumia nguvu wakati wote ni kweli hawafai na wanapaswa wakose imani nao kwani hivi sasa jeshi hilo limebadilika katika kutuangalia sisi wapinzani sio kama zamani ingekuwa zamani siku ile angekufa mtu” alisema Ziada.

Ziada aliwataka wanasiasa kisiwani Pemba kutumia nafasi zao za kujijenga kisiasa zaidi kwa kutafuta wanachama badala ya kutumia vyombo vya kiserekali kuwalazimisha wanayoyataka wao.

No comments:

Post a Comment