Monday, October 5, 2009

Kidato cha nne waanza mtihani leo

Idadi ya wanafunzi walioandikishwa kufanya mtihani wa kidato cha nne unaoanza leo imeongezeka kutoka wanafunzi 241,472 mwaka jana hadi 351,958 wakiwemo wavulana 183,755 na wasichana 168,203.

Idadi ya wanafunzi waliojiandikisha kufanya mtihani huo mwaka huu imeongezeka kwa wanafunzi 110,486 sawa na asilimia 45.7 ya wanafunzi, ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi waliojiandikisha kufanya mtihani huo mwaka jana ambao walikuwa 241,472.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe jana ilieleza kuwa jumla ya watahiniwa wa shule waliojiandikisha kufanya mtihani huo mwaka 2009 ni 254,355 wakiwemo wasichana 116,806 sawa na asilimia 45.92 huku wavulana wakiwa 137,549 sawa na asilimia 54.08.

Ilieleza kuwa mwaka 2008 watahiniwa wa shule waliojiandikisha kufanya mtihani huo walikuwa 166,443 na kusisitiza kuwa mwaka huu kumekuwa na ongezeko la watahiniwa wa shule 87,912 sawa na asilimia 52.82.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kuna ongezeko la watahiniwa wa kijitegemea 22, 574 sawa na asilimia 30.09. Ongezeko hilo linatokana na mwaka huu kujiandikisha watahiniwa 97,603 ikilinganishwa na watahiniwa 75,027 waliojiandikisha kufanya mtihani huo mwaka jana.

Katika taarifa hiyo Maghembe alionya walimu na wanafunzi wanaoiba mitihani mbalimbali na kuwataka kutojihusisha na vitendo hivyo na kusisitiza kuwa watakaobainika kufanya udanganyifu watafutiwa matokeo yao yote kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa mitihani ya taifa.

"Hali hii ya wizi wa mitihani inaweza kusababisha taifa kupata wataalamu wasiokidhi ubora na hivyo kurudisha nyuma juhudi za serikali za kutoa elimu bora kwa wote, wizara inawaasa watahiniwa, wasimamizi, wanafunzi na wananchi wote kujiepusha na vitendo vya udanganyifu wa aina yoyote katika kipindi chote cha mtihani wa kidato cha nne," alisema Maghembe na kuongeza;

"Yeyote atakayebaini ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji wa mitihani asisite kutoa taarifa, yeyote atakayekamatwa atachukuliwa hatua kali za kisheria na kinidhamu."
Aidha Maghembe alieleza katika taarifa hiyo kuwa jumla ya watahiniwa 24,979 wamejiandikisha kufanya mtihani wa maarifa mwaka huu ambao utafanyika Oktoba 9, kati ya wanafunzi hao wasichana ni 14, 702 sawa na asilimia 58.86 na wavulana 10, 277 sawa na asilimia 41.12 mwaka 2008.

Katika mtihani huo watahiniwa wa kujitegemea waliojiandikisha walikuwa 23, 266 kutokana na idadi hiyo kumekuwa na ongezeko la watahiniwa wa maarifa 1, 713 sawa na ongezeko la asilimia 7.36.

No comments:

Post a Comment