Thursday, October 22, 2009

Mauaji ya Albino hayajaisha

Mwanafunzi wa darasa la pili mwenye ulemavu wa ngozi (albino) aitwae Gasper Elikana (10),juzi ameuawa na watu wasiojulikana na kisha kukatwa mguu wake wa kulia na kutoweka nao sehemu ambayo haikujulikana.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Elias Kalinga, alisema tukio hilo lilitokea juzi, majira ya saa 2:30 usiku, katika kijiji cha Wilimilwa wilayani Geita.

Alisema watu hao kabla ya kufanya unyama huo walimjeruhi baba wa kijana huyo kwa kutumia mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na hivyo kupelekea kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa matibabu na hali yake ni mbaya.

Kamanda Kalinga alimtaja baba wa marehemu kuwa ni Elikana Kaswahili (40), ambapo alijeruhiwa wakati akijaribu kupambana na wauaji hao ili kumuokoa mtoto wake lakini hakufanikiwa.

Alisema tukio hilo lilitokea ndani ya nyumba yao baada ya kula chakula cha jioni na watu hao walivamia na kufanikiwa kuingia ndani kwa kuwa mlango ulikuwa haujafungwa kwa kipindi hiko.

Kutokana na hali hiyo Jeshi la Polisi mkoani humo limetangaza zawadi nono ya Shilingi milioni moja za kitanzania kwa mtu yeyote atakayewezesha kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu hao.

No comments:

Post a Comment