Thursday, October 22, 2009

Mbunge wa Ludewa aanguka ghafla mgodi wa Buzwagi

Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Profesa Rafael Mwalyosi juzi alidondoka ghafla wakati kamati hiyo, ilipokuwa ikikagua mgodi wa Buzwagi ulio wilayani Kahama mkoani hapa.

Profesa Mwalyosi, ambaye ni mbunge wa jimbo la Ludewa mkoani Iringa kwa tiketi ya CCM alidondoka majira ya mchana, muda mfupi baada ya kumaliza kikao cha ndani na viongozi wa kampuni ya Barrick Gold inayomiliki mgodi huo, kikao ambacho kilijadili mambo yanayohusu migogoro ya wananchi katika eneo hilo.

Kabla ya kudondoka, mbunge huyo alionekana pembeni akiongea na simu ya mkononi wakati wenzake wakikagua bwawa la maji machafu lililojengwa na Barrick kwa ajili ya kupaulishia maji kutoka eneo la uzalishaji wa dhahabu.

Kwa mujibu wa meneja wa uhusiano wa Barrick inayomiliki mgodi huo, Teweli Teweli, baada ya mbunge huyo kuanguka alilazwa kwa muda katika zahanati iliyo kwenye mgodi huo, baadaye alichukuliwa na ndege ya Barrick na kupelekwa hospitali ya Agha Khan jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Kabla ya kuanguka kwa mbunge huyo, kamati hiyo ilihoji mambo mbalimbali ikiwemo migogoro ya wananchi waliohamishwa kupisha shughuli za kampuni hiyo ya Canada.

Wabunge hao wakiongozwa na mwenyekiti wao, Job Ndugai, ambaye ni mbunge wa Kongwa mkoani Dodoma, walihoji uhalali wa kiwango cha malipo ya fidia kwa wananchi wa Mwendakulima ambao wanailalamikia serikali kushindwa kushughulikia madai yao kwa Barrick.

Hata hivyo, ofisa wa maendeleo ya jamii na mahusiano wa Buzwagi, Benard Mihayo alisema serikali iliunda kamati maalum iliyoshirikisha wananchi wenyewe kwa lengo la kuhakiki madai yao na kwamba ilibainika asilimia 99.9 ya wananchi wameshalipwa wote.

Mihayo aliwaambia wabunge hao kuwa katika kuhakiki madai hayo, iligundulika kuwa ni watu wawili ambao walikuwa wakidai Sh1milioni na mwingine Sh 600,000, ambao wameshasaini fomu na kulipwa, kwa mujibu wa meneja uhusiano wa Barrick, Teweli Teweli.

Mihayo alisema katika wananchi hao wengine 14 wamegoma kwa makusudi kukubali kuwa wameshalipwa licha ya vielelezo vyao kuonyesha wamesaini malipo yao.

Mbunge wa jimbo la Kahama, James Lembeli ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo alihoji uhalali wa Sh287milioni zilizotangazwa bungeni na Waziri wa Nishati na Madini kuwa zimetumika kuwalipa fidia wananchi hao wakati hakuna watu waliolipwa fedha hizo.

Lembeli aliomba uongozi wa mgodi huo umpatie majina yote ya watu waliolipwa fidia hizo ili ayafanyie uchunguzi mwenyewe baada ya kuelezwa kuwa ni watu wawili tu waliolipwa Sh 1 milioni na Sh600,000 hali inayopingana na kauli ya waziri bungeni.

Familia zipatazo 500 kutoka eneo la Mwendakulima zilihamishwa kupisha ujenzi huo wa mgodi wa Buzwagi na kisha kulipwa fidia ikiwemo kujengewa nyumba 207 mbadala lakini baadae wote walilalamika kuwa wamepunjwa katika malipo hayo.
Mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu na kujenga uhasama baina ya wananchi hao na mgodi huo.

No comments:

Post a Comment