Saturday, October 31, 2009

Samaki wa Magufuli kugaiwa bure

Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Bw. John Pombe Magufuli, ametangaza rasmi hatma ya samaki waliokamatwa mikononi mwa maharamia wa nchi za nje katika Bahari ya Hindi kuwa watagaiwa bure kwa taasisi mbalimbali za kijamii nchini.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari bungeni Dodoma, Magufuli alisema kuwa serikali imefikia uamuzi huo baada ya kupata ridhaa ya mahakama na kuridhika na ushahidi uliokwishatolewa.
Alisema Samaki hao watagawiwa katika taasisi za kijamii, kama vile hospitali, shule za sekondari, vyuo mbalimbali, magereza, vituo vya watoto yatima lakini si kwa watu binafsi.

Alisema anakaribisha maombi kutoka katika taasisi hizo zilizoorodheshwa ili waweze kupatiwa samaki hao bure na gharama ya kwuatoa Dar es Salaam itakuwa ni ya taasisi binafsi serikali haitgharamia gharama za usafiri.
Pia aliwatoa hofu watanzania kwa kusema samaki hao wapo katika hali salama kwa kuwa walihifadhiwa katika kiwango cha kutosha na walikuwa na uwezo wa kukaa hata miaka miwili bila kuharibika.

Alisema samaki waliopo wanafikia tani 296.32, kuwa na thamani kubwa ya sh. bilioni mbili na samaki hao wanatarajiwa kuliwa na watanzania milioni moja na serikali haiwezi kufanya biashara kwa kuwauza kwa kuwa kufanya hivyo hakutaleta manufaa yaliyokusudiwa ya kuwafanya Watanzania wanufaike na rasilimali zao.

Samaki hao walikamatwa kutoka Meli yaTouriq One katika Bahari ya Hindi ambapo raia wa kigeni walikuwa wakijishughuslisha na uvuvi haramu ndani ya nchi.

No comments:

Post a Comment