Friday, October 23, 2009

Watanzania waonywa kuhusu dawa za Malaria

Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini TFDA, imewataka watanzania na jamii kwa ujumla kuwa macho na matumizi ya dawa za malaria kwa kuwa kuna dawa feki za malaria zimetengenezwa na kusambazwa mitaani.

Taarifa hiyo iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Magreth Ndomondo, na kusema dawa hiyo imesambazwa mitaani hali ambayo inahatarisha maisha ya watumiaji.
Amesema kuwa dawa hiyo aina ya Duo-Co Tecxin yenye namba ya toleo 820308 ilitengenezwa Novemba 26, 2007 na mwisho wa matumizi yake ni ni Oktoba 26, 2010 imetengenezwa na wimbi la watengenezaji feki wa dawa na kusambazwa kwa wingi mitaani.

Mkurugenzi huyo amesema kasha halisi la dawa hiyo limeandikwa kwa lugha ya Kifaransa na kuna jina la kibiashara na jina halisi la dawa hiyo.Lakini dawa hiyo feki imeandikwa pia kwa lugha ya Kifaransa lakini jina halisi la dawa hiyo halijaandikwa kwenye kasha ya dawa hiyo.

Amesema tofauti nyingine inayopatikana katika dawa hiyo ni kuwa dawa halisi imeandikwa tarehe ya kutengenezwa na tarehe ya kuisha muda wake wa matumizi na namba ya toleo vimechapishwa kwa muhuri wa moto unaosomeka vizuri, lakini dawa feki haina tarehe halisi ya kuisha muda wa matumizi na namba ya toleo vimechapishwa kwa muhuri wa moto usiosomeka vizuri.

Pia dawa halisi ina maandishi nyuma ya kasha na jina la dawa na kiasi cha dawa pamoja na jina la mtengenezaji ambavyo vyote vinasomeka na kuonekana vizuri katika eneo lenye vidonge wakati feki vitu vyote hivyo havionekani vizuri.

Tofauti nyingine ni kwamba vidonge vina rangi ya bluu iliyokolea na upande mmoja kuna mstari katikati na upande wa pili kuna neno D.C.
Vyote hivyo vinasomeka vizuri wakati ile feki haisomeki vizuri.Ndomondo amesema karatasi yenye maelezo ya dawa ina urefu wa sentimeta 21 na upana wa sentimeta 15.5.

Upande mmoja umechapishwa kwa lugha ya Kiingereza na mwingine ni Kifaransa, lakini dawa feki ina urefu wa sentimeta 13.9 na upana wa sentimeta 10.4 na pia upande mmoja umechapishwa kwa lugha ya Kiingereza na mwingine hauna maandishi.

Hivyo ameitaka jamii kuwa makini na tofauti zilizoainishwa naye ili waepuke kununua dawa hiyo ambayo itaweza kuwaletea madhara makubwa baada ya kuitumia.
Pia amewataka wamiliki wa maduka ya dawa kuhakikisha wananunua dawa katika maeneo yaliyosajiliwa na TFDA na kutoa taarifa haraka iwezekanavyo pale wanapohisi kuuziwa dawa hiyo bandia.

Amesema mamlaka hiyo hiyo kwenye juhudi ya kumsaka mtoaji dawa hiyo wakishirikaina na nguvu ya dola ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria

No comments:

Post a Comment