Friday, November 27, 2009

Mbunifu wa kitotoleo kisichotumia umeme

Ufugaji wa kuku ni miongoni mwa shughuli nyingi za kiuzalishaji zinazofanywa na Watanzania zikilenga kuinua uchumi wao.

Hata hivyo kazi hii ambayo imeonekana kukubalika na Watanzania wengi inakumbwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na uagizaji wa kuku na mayai pamoja na vifaa mbalimbali kutoka nje ya nchi.

Katika harakati za kupunguza gharama iwe ndogo na matumizi yawe ya chini kwa mtumiaji kulingana mazingira anayoishi, Mtanzania wa kwanza Shabani Singa ni mbunifu aliyebuni chombo hiki Mgana Incubeta ambayo imerahisisha katika mchakato wa utotoaji wa mayai ya kuku.

Hiki ni kifaa kilichoundwa kwa mfumo wa Hewa-joto kwa ajili ya kuangulia mayai ya ndege aina zote.
Kifaa hiki huweza kumfikia kila mfugaji kwa namna moja au nyingine, ikilinganishwa na uhaba wa upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya aina hiyo uliopo katika mazingira ya sasa.

Wengi hujiuliza kuwa chombo hicho kinatumikaje wakati vijijini hakuna umeme? Singa anaeleza kwa kirefu kuhusu chombo hicho ambacho ni tofauti na Incubeta nyingine za umeme.

"Mgana Incubeta hutumia mafuta ya taa, aina yoyote ya gesi na hata mkaa, umeme unapokatika kwa dharura na kwa muda mrefu kiasi cha kuhatarisha mayai yaliyo tayari ndani ya Incubata hii husaidia kuondokana na tatizo hilo," anasema Mgana.

kifaa hicho ni tofauti na Incubeta nyingine za umeme ambazo viungo vyake vya kugeuzia mayai (Auto Egg Turning) vikipata tatizo hufanya Incubata isiweze kutumika.

Anaeleza kuwa kifaa hicho alikitengeneza kwa ajili ya matumizi yake ya nyumbani, kilianza kutumika kwa kutumia mkaa na mafuta ya taa katika kuatamia mayai ya kuku wake wa nyumbani.

Mali ghafi anazotumia katika kukiendesha kifaa hicho, zinapatikana katika sehemu zote za Tanzania hivyo kukipa uwezakano mkubwa wa kutumika mahali popote nchini.

Kifaa hicho amekitengeneza kwa kutumia mbao na zulia ambavyo ni vitu asili, vinatengenezwa kutokana na mazingira ya Tanzania kwa sababu hakuna uhakika wa umeme.

Hata hivyo anasema kuwa kimeundwa kwa kulenga kutumia gharama ndogo kwani kinatumia mafuta lita 5 hadi 10 kwa siku 21, ambayo ni gharama ndogo ukilinganisha na uwezo wake wa kazi na faida inayozalishwa.

Anasema kuhusu umri wa kifaa hicho inategemea uangalifu wa mtumiaji sehemu ya kiungo muhimu ambacho ndiyo moyo wa chombo kinaweza kudumu zaidi ya miaka 10.
Viungo vingine vinaweza kubadilishwa kwa urahisi na kwa gharama ndogo.

Singa anasema kuwa chombo hiki kimeundwa kwa vifaa vinavyozalishwa nchini. Kimeundwa kwa ufundi rahisi kumwezesha mtu yeyote kukiendesha kwa ufahamu mdogo wa kitaalamu.

Anasema kwa kutumia chombo hiki, faida ya mfugaji wa ndege (kuku) huongezeka zaidi ya mara kumi.
Anasema uzoefu unaonyesha kuwa kwa wastani kuku wa kienyeji hutaga mayai 15 kwa uzazi mmoja, huatamia kwa siku 21, hulea vifaranga wake kwa siku 90 na kupumzika kwa siku 10 hadi 15 kabla ya kuanza kizazi kingine.


"Kwa hiyo kizazi au kipindi kimoja huchukua siku 15 kutaga, ukiongeza siku 21 kuatamia na ukiongeza siku 90 ya kulea vifaranga pamoja na siku 15 za kupumzika siku 141 isiyozidi mikupuo 3 ambayo ni sawa na vifaranga 45 kwa mwaka mzima," anasema na kuongeza kuwa;.

"kuku huyo ukimtumia kwa njia ya kisasa anayetaga mayai 15, usimruhusu ayaatamie, utayachukua mayai na kuyaweka kwenye chombo (Mgana Incubeta) ili yatotolewe, atapumzika siku 15 na kuanza kutaga mkupuo mwingine iwapo hataruhusiwa kuatamia mayai yake.

Hivyo kwa kizazi au kipindi kimoja huchukuwa siku 15 za kutaga, 15 za kupumzika kabla ya kizazi kingine. Jumla siku 30."

Singa anaendelea kusema kuwa angefurahi kama angeweza kupanua ujuzi wake ili atoe ajira kwa vijana wanaoishi katika mazingira magumu.
Aidha anasema Serikali ingejaribu kuwekeza macho kwa wenye vipaji maalumu ili kuwainua na kushirikiana nao.
Mbunifu wa kifaa hicho cha kutotoleshea mayai ya kuku wa kisasa na wa kienyeji, alizaliwa miaka 48 iliyopita mkoani Pwani, amesoma shule ya msingi ya Boko na sekondari ya Njombe na kumaliza kidato cha sita Sekondari ya Kibaha.


Baada ya hapo alijiunga na chuo cha Afya na Mifugo Livestock Training Istitute (LITI) cha Arusha.


Mwaka 2007 aliamua kujiajiri mwenyewe na kujikita katika kwenye bidhaa za ufugaji wa kuku,na kutengeneza mashine ya kuatamia mayai na kutoa vifaranga (Mgana Incubeta), na aliizindua rasmi na kuitwa MGANA POULTRY POINT ambayo ofisi yake ipo Mbezi barabara ya Tegeta 'A' jijini Dar es Salaam.

6 comments:

  1. Hujajjiweka wazi kimawasiliano tutakupataje na kifaa hicho ni bei gani? Nina maswali mengi ya kujifunza toka kwako.

    ReplyDelete
  2. hata mimi ningehitaji kukuona mkuu

    ReplyDelete
  3. mawasiliano yake ili tumppate, tunahitaji

    ReplyDelete
  4. Upatikanaji wake ni was namna gani kwa wakazi was arusha

    ReplyDelete