Monday, November 9, 2009

Moto wateketeza Maisha Club Dar

Moto mkubwa ulizuka jana adhuhuri na kuteketeza kabisa klabu maarufu ya usiku jijini Dar es salaam ya Maisha iliyo Oysterbay wilayani Kinondoni.
Moto huo, ambao chanzo chake kimeelezwa kuwa ni hitilafu ya umeme iliyoanzia katika kiyoyozi (AC), ulilipuka na kusambaratisha kabisa jengo la klabu hiyo na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha.


Jengo hilo la ghorofa moja linalomilikiwa na Watanzania wenye asili ya Kiasia, lilianza kushika moto majira ya adhuhuri jana na kuteketeza kabisa mali zote zilizokuwamo ndani yake.

Klabu hiyo kongwe na inayosifika kwa mambo ya burudani mbalimbali na biashara za usiku, ipo mkabala na Hoteli ya Karibu, eneo linalotambulika zaidi kwa jina la Morogoro Store.

kikosi cha zimamoto cha kampuni ya Knight Support kilijitahidi kuzima moto huo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, meneja wa klabu hiyo, Tongai Muza alisema moto huo ulianzia kwenye kiyoyozi kilicho sehemu ya baa katika jengo hilo na baadaye kusambaa sehemu mbalimbali.


"Tuliwapigia simu watu wa zimamoto, lakini walikuwa hawapokei, baadaye AC ikaanza kutoa moto," alisema Muza.
"AC hii ilikuwa inasumbua kwa muda mrefu na ilishughulikiwa na ikatulia kabisa, lakini leo (jana), majira ya adhuhuri ikaanza kutoa moshi. Moto ulianza saa 7:45 mchana na zimamoto walifika saa 8:30 mchana."


Akizungumza kwa unyonge Muza alifafanua kuwa hasara ni kubwa iliyopatikana kutokana na moto huo kwa sababu vito vyote vilivyokuwamo kwenye klabu hiyo ya kisasa viliteketea kwa moto, isipokuwa televisheni moja, mashine ya DVD na Sh700,000 ambazo walibahatika kuziokoa.

"Kama kungekuwa na mwitikio wa haraka kwa vikosi vya zimamoto basi hasara hii isingepatikana, kwa sababu sisi tuliwahi kutoa taarifa," alisema Muza.
Muza alivitaja baadhi ya vitu vilivyokuwamo ni pamoja na sofa, TV, spika, redio, AC, vifaa vya kudhibiti mwanga, vinywaji na samani nyingine mbalimbali ambazo huwekwa kwenye kumbi za burudani, hasa kumbi za disko.


Mmiliki wa kampuni ya Entertainment Master, Hellen Swea ambaye ni mpangaji wa jengo hilo, alishindwa kuzungumza lolote kuhusu tukio hilo kutokana na machungu ya kupotelewa na mali zake.

Sweya, ambaye ni mstaafu, muda wote alionekana akifuta machozi huku watu mbalimbali wakimfariji kwa kumkumbatia na kumpa pole.
"Mama anasema hawezi kuzungumza na vyombo vya habari kwa leo," alisema mtoto wake wa kike ambaye alikuwapo eneo la tukio.


Kwa upande wake mmoja wa watoto wa mmiliki wa jengo hilo, Dibesh Dibecha alisema cha kwao ni jengo tu lakini mali na vitu vyote vya samani ni vya mama Sweya ambaye ni mpangaji.

Kwa mujibu wa mashuhuda kuteketea kabisa kwa jengo hilo kulisababishwa na kuchelewa kuwasili kwa vikosi vya zimamoto na ufinyu wa miundonu ya jengo hilo la ghorofa moja.
Magari ya zimamoto yalilazimika kusimama umbali wa mita 40 na hivyo kufanya kazi yao iwe ngumu.
Kikosi cha zimamoto kilifika eneo la tukio, saa 9:22 alasiri na kuambulia mayowe na kuzomewa na watu mbalimbali waliokuwa wakishuhudia tukio hilo.

Mkurugenzi wa kampuni ya African Stars Entertainment, Asha Baraka alisema alikuwa ni miongoni mwa watu waliopata taarifa za moto huo mwanzoni na kwamba alihangaika sana kupiga simu kwa vyombo mbalimbali vya habari ili kuomba msaada wa kusambazwa kwa taarifa hizo.

"Juhudi zangu na za wenzangu hazikufanikiwa kuiokoa Maisha Club na hatimaye yote imeteketea.
Klabu hii kwa kweli imewainua wanamuziki wengi hata African Stars imefanya kazi hapa kwa miaka 10," alisema Baraka.

"Mimi namsikitikia sana mama Sweya ni mstaafu, mdau na msikivu sana kwa watu wote wanaomshauri. Nashindwa kuzungumza zaidi siwezi," aliongeza.

Kamanda wa polisi mkoani Kinondoni, Mark Kalunguyeye alisema kwa sasa wanaendelea na kukusanya taarifa kwa ajili ya uchunguzi na kwamba watakapomaliza watatoa taarifa kamili juu ya chanzo cha moto huo.

Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Oysterbay, Peter Mushi alisema kuungua kwa klabu hiyo kumepoteza mapato kwa serikali yake na ajira za wakazi wake.

No comments:

Post a Comment