Monday, December 14, 2009

Safari ya Denmark ilikuwa ya Dk Shein---Ikulu

Ofisi ya rais imesema safari ya Makamu wa Rais Dk Ali Mohamed Sheni kwenda Copenhagen, Denmark iliandaliwa tangu awali kwa ajili yake na wala haikuwa ya Rais Jakaya Kikwete.

Imesema safari hiyo ya kuhudhuria mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, iliratibiwa kuhudhuriwa na Dk Shein kwa kuwa ofisi yake ndiyo inayoshughulikia masuala ya mazingira.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu Salva Rweyemamu alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba haikuwa imepangwa kwa Rais Kikwete kuhudhuria bali Dk Shein.

Rweyemamu alisema hayo wakati akifafanua taarifa zilizoripotiwa jana na vyombo vya habari kuwa Rais Jakaya Kikwete amebadili uamuzi wa kwenda Copenhagen, Denmark kuhudhuria mkutano huo na kumtuma makamu wake Dk Shein.

"Si kweli kabisa kwamba Rais Kikwete ameshindwa kuhudhuria, tokea awali Dk Shein ndiye alipangwa kuhudhuria mkutano huo, yeye ndiye anahusika na mazingira," alisema Rweyemamu.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa juzi jijini Dar es Salaam ilieleza kuwa katika mkutano huo makamu wa rais ataongoza ujumbe wa Tanzania unaojumuisha mke wake, Mama Mwanamwema Shein, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dk Batilda Burian na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Mazingira wa Zanzibar, Bruhani Haji Saadat.
Dk Shein na ujembe wake waliondoka jana nchini kuhudhuria mkutano huo.

No comments:

Post a Comment