Friday, April 9, 2010

Ardhi ya Tanzania yamegwa mpakani

Kila mwaka mipaka ya Tanzania inamegwa na nchi jirani za Malawi, Zambia, Msumbiji na Kenya kwa kuingia ndani zaidi.
Hayo yalielezwa jijini Dar es Salaam jana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilipokutana na watendaji wakuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika ofisi ndogo za Bunge.

Mjumbe wa kamati ya PAC, Ponsiano Nyami ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Nkasi mkoani Rukwa alisema kuwa nchi zinazopakana na Tanzania kila mwaka zimekuwa na tabia ya kung'oa mawe (beacon) yaliyopo mpakani na kuyasogeza ndani ya ardhi ya Tanzania kwa siri.

"Hivi nyie watendaji wa Wizara ya Ardhi, mnajua kuwa mipaka yetu inaibwa na nchi tunazopakana nazo?" alihoji Nyami na kuongeza:

"Ukienda kuangalia mawe ya mipaka yote hayapo katika mahala pake pa asili.
Kila mwaka nchi tunazopakana nazo zimekuwa na tabia ya kung'oa beacon na kuzisogeza ndani ya Tanzania kwa zaidi ya kilometa moja na kuendelea".

"Haya ninayosema ni ya kweli na nimeyashuhudia kwa macho yangu mwenyewe hasa katika mpaka wa Kaskazini mwa nchi yetu".

Kaimu Mkurungezi wa Upimaji na Ramani wa Wizara hiyo, Dk Silassie Mayunga alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kusema kuwa alama nyingi za mipaka zimeondolewa na nchi hizo.

Dk Mayunga alifafanua kwamba, kutokana na hali hiyo serikali kupitia wizara hiyo ipo katika utaratibu wa kupima upya mipaka hiyo na kwamba, tayari imekwishafanya mazungumzo na nchi husika kuhusu hali hiyo.

"Ni kweli alama nyingi za mipaka zimeondolewa na nchi tunazopakana nazo na nyingi zimeingia ndani ya ardhi yetu. Serikali kupitia wizara ipo katika utaratibu wa kupima upya mipaka yetu na tayari tumekwishafanya mazungumzo na nchi husika kuwajulisha kuhusu hali hiyo," alisema Dk Mayunga.

Bila kufafanua zaidi, Dk Mayunga alisema katika mpaka wa Kenya kilometa 325 ndio zilizobakia kupimwa na upande wa Msumbiji upimaji umekwishaanza.

"Mpaka wa Msumbiji tayari tumekwishaanza kuupima, lakini katika mpaka wa Kenya zimebakia kilometa 325 kupimwa,"alisema Dk Mayunga,

Kuhusu mpaka na Malawi, Dk Mayunga alisema upimaji bado haujaanza na kwamba wapo katika mazungumzo kuhusu eneo halisi la umiliki.

Kuhusu mpaka wa Zambia, Dk Mayunga alisema: mazungumzo yanaendelea vizuri.

"Kwa upande wa Zambia mazungumzo yamekamilika, lakini kwa upande wa Malawi upimaji bado haujaanza, tunaendelea na mazungumzo kuhusu eneo halisi la umiliki,"alisema Dk Mayunga.
Dk Mayunga alisema pamoja na kung'olewa kwa mawe ya mipaka baadhi ya sehemu yamekwisha rudishwa.


Awali, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Patrick Rutabanzibwa alisema tangu nchi ipate uhuru mipaka ya nchi haijapimwa.
"Ukweli ni kuwa mipaka ya nchi ilifanyika kabla ya nchi haijapata uhuru na baada ya kupata uhuru haijawahi pimwa,"alisema Rutabanzibwa.


Rutabanzibwa alisema wizara inatumia michoro ya ramani ya zamani katika kurudisha mawe ya mipaka.

No comments:

Post a Comment