Monday, May 3, 2010

serikali ya Tz na mgomo wa wafanyakazi

Wakati wafanyakazi kupitia Shirikisho lao Tucta wakitaka utekelezaji wa vitendo kwa kupunguzwa kodi ya mapato kwa watumishi wa umma, serikali imezidi kutoa ahadi ikisema taarifa juu ya hilo itatolewa Mei 8 mwaka huu.

Tayari Tucta imeapa kuendelea na mgomo huo kuanzia Mei 5 huku juzi ikiadhimisha siku ya Wafanyakazi Duniani mbele ya viongozi wa kambi ya upinzani kwenye uwanja wa uhuru, ikiwatenga viongozi wa serikali.

Licha ya Tucta kutangaza kuanza mgomo Mei 5, bado serikali imezidi kutoa ahadi baada ya kutoa taarifa ya matangazo katika vyombo vya habari ikisema suala la kupunguzwa kodi ya mapato kwa watumishi wa umma limejadiliwa na litatolewa majibu ifikapo muda huo.

Mwenyekiti wa Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma Anastasia Mmuni, alisema katika mkutano wao wa Aprili 27 hadi 30 uliofanyika Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma, suala hilo lilijadaliwa kwa kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi hiyo kutoka asilimia 15 hadi 13.

" Ilikubaliwa kwamba taarifa itolewe kwenye mkutano wa Baraza uliopangwa kufanyika tarehe 8 Mei, 2010." Hata hivyo, kwa ahadi hiyo tayari mgomo utakuwa umeanza Mei 5, alisema.


Juzi Tucta wakati wa Mei Mosi, ilisisitiza kwamba inataka utekelezaji wa vitendo wa kupunguzwa kodi ya mapato kwa watumishi wa umma vinginevyo mgomo huo utafanyika kama ulivyopangwa.

Kuhusu Mafao ya Hitimisho la Kazi, Mmuni alitoa ahadi, akisema serikali imeahidi kuhakikisha Mdhibiti na Msimamizi wa Hifadhi ya Jamii atakuwa amepatikana baada ya kuteuliwa ifikapo Septemba 30, 2010 ili aweze kutekeleza majukumu.

Mwaka 2008, Bunge lilipitisha Sheria Namba nane ya Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii, ambayo inalenga kuiweka mifuko ya hifadhi ya jamii chini ya mamlaka moja ya usimamizi.

Akizungumzia nyongeza ya mishahara ya watumishi wa umma kwa mwaka 2010, alisema wajumbe walikubaliana kutokubaliana kuhusu kiwango cha kima cha chini cha mishahara.

"Kwa kuwa wajumbe walikubaliana kutokukubaliana kuhusu kiwango cha kima cha chini cha mshahara, walikubaliana kuwasilisha makubaliano ya kutokukubaliana kwa waziri mwenye dhamana ya utumishi wa umma," alifafanua Mmuni.

Alifafanua kwamba, kwa mujibu wa sheria hiyo makubaliano ya Baraza yatawasilishwa kwa waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma kwa uamuzi au maelekezo ya namna ya kushughulikia suala la nyongeza ya mishahara mwaka 2010/11.

Mgomo wa Tucta umeingiza nchi katika historia mpya baada ya wafanyakazi kugawanyika katika vyama viwili, huku upande mmoja ukialika viongozi wa serikali na mwingine kuhudhuriwa na kambi ya upinzani akiwemo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa.

No comments:

Post a Comment